Yanga na Simba zavimbiana Dar

Monday February 13 2017

 

By IMANI MAKONGORO

TAMBO za mashabiki wa Simba na Yanga zimeanza kuelekea kwenye mchezo wao wa Februari 25, huku Yanga ikiwakejeli wenzao kwa kuwaambia sio saizi yao kisoka kwani timu yao imezoea kushindana na mabingwa wa Afrika na si timu ya mtaani.

Mashabiki wa timu hizo wameanza maandalizi mapema ili kutoa hamasa kwenye timu zao kuelekea kwenye mchezo huo huku kila mmoja akijiaminisha timu yake kuchukua pointi zitakapokutana kwa mara ya pili msimu huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mzunguko wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya 1-1, huku mashabiki wa Simba waking’oa viti baada ya refa kumpa kadi nyekundu Jonas Mkude sambamba na

kulalamikia bao la Amissi Tambwe ambalo alifunga baada ya kuumiliki mpira kwa mkono.

Kwa nyakati tofauti jana Jumapili, mashabiki wa timu hizo walitambiana huku wale wa Simba ambao timu yao imerejea kileleni kwenye msimamo ikiwa mbele kwa mechi moja dhidi ya Yanga wakijinadi kutoshuka huku Yanga wakiwakejeli kwamba sio saizi yao.

“Unajua Yanga tulishazoea ushindi hivyo tunaichukulia Simba kama timu ya mtaani tu wala haitupi presha kwanza si saizi yetu kabisa kwani mabingwa wote wa Afrika wikiendi hii wako viwanjani wanashindana kimataifa.

“Hatuhangaiki na timu ya mtaani na bahati nzuri nao wanalijua hilo kwamba ni wa mtaani, Simba ni kama sikio haliwezi kuzidi kichwa,” alitamba katibu wa matawi ya ushangiliaji ya Yanga, Steven Mwakilema.

Alisema timu yao huwa inajipanga kucheza na mabingwa hivyo kwenye mchezo wao na Simba hawana presha kwani ni kawaida yao kuifunga na kutwaa ubingwa sambamba na kuiwakilsha nchi kimataifa.

Upande wa Simba, Mwenyekiti wa Kundi la Ushangiliaji la Wekundu wa Terminal, Joel Mwakitalima alisema safari hii Yanga watalitafuta goli la mkono bila mafanikio.

“Hatutaki kuongea sana sababu tunajiamini, tusubiri siku ya mechi si wamezoea magoli yao ya mkono, sasa safari hii wajipange kweli kweli,” alisema.

Wakati mashabiki wakiendelea na tambo hizo, Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja aliliambia gazeti hili jana Jumapili kwamba wanachokifikiria ni pointi tatu katika mechi zao zote ikiwamo ya Yanga.

“Tumepanda juu kwenye msimamo, lakini tuko mbele mechi moja kwa Yanga, tunahitaji ushindi kwa asilimia 100 tutakapocheza nao ili kuendelea kukaa kuongoza ligi na hatimaye kutimiza ndoto yetu ya kutwaa ubingwa,” alisema Mayanja.

Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisisitiza kwa kusema kwamba timu hiyo itacheza mechi zote kama fainali na kwa kusaka pointi tatu ili kuweza kutetea taji hilo msimu huu.