Yanga inakamilisha ratiba saa 10

Muktasari:

  • Hesabu zao zimeshabuma kitambo na wamekatwa, wanachofanya ni kupasha tu kujiweka sawa na msimu ujao wa Ligi ya Mabingwa pamoja na Ligi Kuu Bara.

HATA Yanga ikishinda mabao 10-0 pale Lubumbashi hayawezi kuisaidia. Wanakamilisha ratiba tu ya mechi za hatua ya makundi za Kombe la Shirikisho Afrika leo Jumanne wakapocheza na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hesabu zao zimeshabuma kitambo na wamekatwa, wanachofanya ni kupasha tu kujiweka sawa na msimu ujao wa Ligi ya Mabingwa pamoja na Ligi Kuu Bara.

Yanga ina pointi nne tu katika mechi tano za awali huku Mazembe wakifuzu baada ya kukusanya pointi 10 wakati Medeama ya Ghana inahitaji angalau sare tu ili kuweza kuungana na Mazembe katika kundi A.

Katika mchezo huo Yanga inasaka ushindi ili kulipa kisasi cha kipigo cha bao 1-0 ilichopokea katika mchezo wa raundi ya kwanza, Dar es Salaam huku pia wakipiga hesabu za kushinda ili kujiweka karibu na mkwanja mkubwa wa Caf.

Yanga mpaka sasa ina uhakika wa dola 165,000 (Sh 354 milioni) kama itamaliza katika nafasi ya nne, lakini endapo itafanikiwa kumaliza nafasi ya tatu itapata dola 259,000 (Sh 554 milioni). Kabla ya kuondoka nchini juzi Jumapili alfajiri, kocha wa Yanga, Hans Van Pluijjm, alisema wanaupa uzito mchezo huo kwa kuwa ni sehemu nzuri kwao kulipa kisasi huku wakilinda heshima ya Yanga pia.

“Tusisahau kuwa walitufunga hapa mchezo wa awali, tunakwenda kusaka heshima Kongo, tunataka kushinda ili kulipa kisasi na kulinda heshima yetu pia, kwangu kila mchezo ni muhimu,” alisema Pluijm.