Yanga Mwanza ni makundi Afrika

Muktasari:

Meneja wa Uwanja wa Kirumba, Steven Shija, amesema katika ukaguzi wa uwanja uliofanywa kwa siku mbili na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kupitia ofisa wake, Maxwell Mtonga, raia wa Malawi, kuna dosari kadhaa zimebainika ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi ambapo endapo nusu ya hizo zikikamilika mpaka kufikia Aprili 10 wataruhusu mechi za Yanga kufanyika katika uwanja huo.

YANGA ilipanga kuhamishia mechi zake za kimataifa katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, lakini uhalisia ni kwamba hakuna haraka inayoweza kufanya kuiwahi mechi dhidi ya MC Alger ya Aprili 8. Italazimika kusubiri hatua ya makundi.

Meneja wa Uwanja wa Kirumba, Steven Shija, amesema katika ukaguzi wa uwanja uliofanywa kwa siku mbili na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kupitia ofisa wake, Maxwell Mtonga, raia wa Malawi, kuna dosari kadhaa zimebainika ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi ambapo endapo nusu ya hizo zikikamilika mpaka kufikia Aprili 10 wataruhusu mechi za Yanga kufanyika katika uwanja huo.

“Kuna mambo wametuambia tuyafanyie kazi, walikagua sehemu ya kuchezea kuna maeneo wametutaka kuyafanyia kazi kusawazisha na kupanda nyasi, pia katika magoli pia kuna maelekezo wametupa,kuna vyumba tumeambiwa tuvifanyie marekebisho tumeambiwa tutenge chumba maalumu cha ofisa wa CAF na chumba cha dharura cha matibabu, hivyo vyumba vipo lakini kuna maboresho tutayafanya,”alisema Shija.

“Ukiacha hivyo pia vyoo vya jumuiya navyo tumepewa kazi ya kuvifanyia marekebisho ili viwe na hadhi ya kimataifa hata nyie wanahabari pia tumeambiwa tuwawekee chumba maalumu kitakachokidhi kufanya majukumu yenu na hayo yote wamesema tukiyakamilisha hata nusu yake kabla ya Aprili 10 watakuja kukagua na kuruhusu uwanja kutumika sasa tunajipanga kutafuta fedha na kuna kazi imeshaanza kufanyika.

“Ninajua kwanini Yanga wanataka kuja hapa, niwahakikishie wakija Kirumba hasa kucheza mchezo wa kimataifa sisi kama wenyeji wao tutawapatia ulinzi ambao utakidhi matakwa yao, najua wanaogopa kufanyiwa hujuma na watani wao kiukweli hatutaruhusu mtu kugusa uwanja kama sio kiongozi wa Yanga na kwa kuwa wanajuana tutashirikiana nao katika kulinda.

“Tunataka kutanguliza uzalendo mbele, hili haijalishi iwe Simba au Yanga, kama Simba nao watakuja kutumia uwanja wetu katika majukumu ya kimataifa hivyo hivyo pia Yanga watakazimika kukaa mbali na uwanja tutawapa nafasi kubwa timu mwenyeji kufanya maandalizi yake kwa uhakika lakini pia ulinzi utakuwepo wa kutosha.”