Wanne wapigwa benchi kubwa Yanga

Lwandamina

KOCHA wa Yanga, George Lwandamina si mtu wa mchezo mchezo, amewatoa nishai baadhi ya mastaa wa timu hiyo kwa kuwachomesha mahindi nje tangu atue Yanga miezi miwili iliyopita.

Lwandamina tayari ameiongoza Yanga katika mechi tisa za mashindano matatu ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Mapinduzi na FA, amewaweka kando wachezaji wanne na kushindwa kuwatumia kabisa katika kikosi chake japo kuwafanya chaguo la pili. Hadi sasa ametumia wachezaji 21 katika kikosi chake huku Malimi Busungu, Obrey Chirwa, Pato Ngonyani na Ally Mustapha ‘Barthez’ wakiwa hawajacheza mechi hata moja ya mashindano. Amekuwa akimtumia kipa Deo Munishi ‘Dida’ aliyedaka mechi nane huku Beno Kakolanya akidaka moja na kumwacha Barthez akichoma mahindi.

Katika beki ya kati, amewatumia Andrew Vincent na Kelvin Yondani na kumfanya, Pato Ngonyani kuwa mwanachama wa kudumu benchi huku Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akicheza mechi moja tu ya Kombe la Mapinduzi tena akitokea benchi.

Matteo alishindwa kumvutia kabisa Lwandamina na kujikuta akiwekwa benchi mechi nane za mwanzo kabla ya kupewa dakika 12 kwenye mechi ya Kombe la FA dhidi ya Ashanti United.

Busungu hajacheza mechi yoyote ya mashindano tangu kutua kwa kocha huyo huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni matatizo yake ya nje ya uwanja ikiwemo kesi ya kusababisha ajali iliyokuwa ikimkabili mjini Morogoro.

Chirwa aliyekuwa majeruhi licha ya kupona bado hakupata nafasi katika mechi ya FA wakati Yanga ikiilaza Ashanti  4-1 hivyo anakuwa amecheza dakika tatu tu za mechi za mashindano chini ya Lwandamina.

OSCAR, MAHADHI

Beki Oscar Joshua ameweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyecheza nafasi nyingi zaidi uwanjani katika kikosi cha Mzambia huyo,  hadi sasa amechezeshwa katika maeneo matatu tofauti.

Joshua kiuhalisia ni beki wa kushoto, alipangwa kucheza straika mechi ya Kombe la Mapinduzi na Zimamoto, alicheza  kiungo dhidi ya Majimaji na beki wa kati dhidi ya Ashanti. Wakati huo huo, Chipukizi, Juma Mahadhi ameshidwa kuitendea haki nafasi ya straika ambayo amekuwa akichezeshwa na Lwandamina, katika mechi tano amefunga bao moja tu.