Wanachama Simba wakimbilia kwa JPM

Monday March 20 2017

By MWANAHIBA RICHARD

WANACHAMA wa klabu ya Simba wamemuandikia barua Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kumuomba awaruhusu kwenda kumuona tena Rais John Magufuli ili asikilize kilio chao kwa madai kuwa klabu yao inataka kuuzwa kinyemela.

Simba ipo kwenye mchakato wa kubadilisha mfumo wa uendeshaji wake, kutoka ule wa wanachama na kuwa kampuni ambapo, itawaruhusu wadau mbalimbali kununua hisa na wanachama hao waliwahi kutinga Ikulu kuonana na Rais Magufuli.

Machakato huo umeanza baada ya bilionea Mohamed Dewji ‘Mo’ kuomba kuwekeza Sh 20 bilioni huku akitaka kumiliki hisa kwa asilimia 51, jambo ambalo linapingwa vikali na baadhi ya wanachama wakihoji sababu za MO kutaka kumiliki hisa nyingi.

Mratibu wa wanachama wazee wa Simba wanaopingana na mabadiliko hayo kwamba, hayajafuata taratibu za kikatiba, Felix Makua aliliambia Mwanaspoti kuwa wameandika barua kwa Nape ili kuomba muongozo wa kuonana na Dk. Magufuli baada ya wao kusikia viongozi wa Simba wamewasilisha Rasimu ya Katiba kwa Msajili wa Vyama vya Michezo wilayani Ilala.

“Tulienda kwa Rais Magufuli mara ya kwanza ili kuzuia mchakato huu usifanyike, hata kwa Nape tulizungumza naye alituahidi kulishughulikia mara tu Rasimu itakapowasilishwa kwake, viongozi wa Simba kuna vitu wanavifanya nyuma ya pazia ambavyo si vizuri ndani ya klabu yetu, haki nyingi zitapotea.

“Huu mchakato hauna elimu yoyote kwa wanachama na wanaokubaliana nao ni wale ambao wanapelekeshwa, tuliambiwa tutaamua mfumo wa kuhamia kwenye mabadiliko ambapo kuna mifumo mingi ila wao Kamati ya Utendaji wamepitisha wenyewe, hiyo sio sawa. Hapa kuna mchezo unaendelea na sio mzuri hata kidogo.

“Kwa kubaini hilo ndiyo sababu tunaomba kwenda kuonana na Dk. Magufuli ili atusaidie kuinusuru klabu yetu yenye, ambayo kwa sasa ina kila dalili na mwelekeo wa kuuzwa,” alisema Makua mwenye kadi ya uanachama namba 05012.