Wamekuja kichovu hivi watakula nyingi Taifa

Muktasari:

Yanga inawakaribisha Ngaya katika mchezo wa marudiano wa hatua ya awali ya Klabu Bingwa Afrika, katika mchezo wa kwanza walishinda kwa mabao 5-1 ugenini Comoro.

KAMA una buku tatu tu leo unaweza kuingia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwatazama Yanga wakicheza mchezo wa kimataifa dhidi ya Ngaya De Mbe ya Comoro na tathmini inaonyesha kuwa watakula mabao ya kutosha hata kama watashangiliwa na Simba.

Yanga inawakaribisha Ngaya katika mchezo wa marudiano wa hatua ya awali ya Klabu Bingwa Afrika, katika mchezo wa kwanza walishinda kwa mabao 5-1 ugenini Comoro. Habari mbaya kwa timu hiyo ya Comoro ni kwamba haijawahi kucheza kwenye uwanja mkubwa kama Taifa, kwani ni timu ngeni anga za kimataifa, lakini pia Yanga wamepania kuwapiga bao nyingi za sifa ili kujiweka sawa na mechi ya Simba.

Rekodi zinaonyesha kuwa Yanga haijapoteza mchezo wowote wa mashindano katika uwanja wa nyumbani msimu huu na katika mechi ya kimataifa imefungwa mara moja tu na TP Mazembe katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alithibitisha kuwa mastaa wao wakubwa, Obrey Chirwa, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma na Amissi Tambwe hawatakuwepo leo kutokana na kusumbuliwa na majeruhi lakini Mwanaspoti linafahamu kuwa wamepumzishwa kwaajili ya mechi dhidi ya Simba itakayochezwa wikiendi ijayo.

Hali hiyo inamaanisha kuwa kiungo Said Juma Makapu, Deus Kaseke, Matheo Antony na Juma Mahadhi wana nafasi ya kuanza katika kikosi cha leo kuziba nafasi hizo zilizoachwa wazi.

“Ushindi wa mchezo wa kwanza umetuweka katika hatua nzuri ya kusonga mbele, ukiachana na wachezaji hao wanne ambao hawako fiti, wengine wote wako vizuri,” alisema Mwambusi ambaye ni kocha wa zamani wa Prisons na Mbeya City.

“Tuliwafunga mabao matano lakini si wabovu sana kama unavyofikiri, tunapaswa kucheza nao kwa tahadhari kubwa,” alisema Tambwe ambaye msimu huu tayari amefunga mabao 12 katika mashindano yote.

 

LIGI KUU NI KESHO

Mechi kali zaidi itakuwa kesho Jumapili kati ya Mwadui watakaokuwa wenyeji wa matajiri wa Juisi, Azam mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Mchezo mgumu zaidi ni wa Mtibwa na JKT Ruvu inayopambana kujinasua na hatari ya kushuka daraja sawa na ule wa Mbao na Majimaji ambazo zote bado hazipo salama katika eneo la kushuka. Ndanda itacheza na African Lyon pia kesho.