Wacongo lazima wakae kwao

SERENGETI Boys juzi Jumapili ilipata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Congo Brazzaville na kuonekana ipo mguu ndani mguu nje katika harakati zao za kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana u17, hata hivyo Kocha Bakar Shime amefichua siri nzito.

Kocha huyo maarufu kama Mchawi Mweusi, amesema Congo lazima ipigwe kwao hata kama ni kweli mwaka 2012 nchi hiyo iliibania Tanzania kwa kuifunga mabao 2-0 ikiwa kwao baada ya kupewa kichapo cha bao 1-0 jijini Dar es Salaam.

Shime alisema ni kweli safu yao ya ulinzi katika mechi ya juzi Jumapili ilipwaya kwa kuwakosa nyota wake wawili waliokuwa wakitumikia adhabu za kadi, mmoja kadi mbili za njano na mmoja nyekundu, lakini katika mechi yao ya marudiano vijana hao watakuwepo na lazima Congo waombe po!

Aliwataja wachezaji aliowakosa juzi na ana uhakika wa kuwatumia mechi ijayo na hivyo kuidhibiti Congo ikiwa kwao ni Dickson Job na kiungo Ally Ng’anzi.

“Nina uhakika timu yangu itafanya vizuri katika mchezo huo, kuna wachezaji ambao hawakucheza mechi  ya juzi kama Ally Ng’anzi na Dickson Job. Hawa ni wachezaji muhimu kikosini kwani wamecheza pamoja kwa muda mrefu na kuisaidia timu,” alisema na kuongeza:

“Kwa mechi ijayo watacheza na kurejesha uimara wa safu yetu ya ulinzi na sioni mahali Congo wataponea, achaneni na rekodi ya mwaka 2012, safari hii tunaamini Tanzania tutaenda fainali za Afrika za Madagascar, tuombeeni Mungu atusaidie.”