Wachezaji wote Simba posho juu

Muktasari:

  • Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya Simba ni kwamba mabosi hao wameanzisha mpango maalum wa kutoa motisha kwa wachezaji wake ambapo imeanzisha utaratibu maalum wa kukusanya kiasi cha fedha ambacho inakitoa kama motisha kwa nyota hao pindi wanaposhinda mechi.

MABOSI wa Simba wamechoshwa na ukame wa mataji unaoendelea klabuni hapo na sasa baada ya kusajili wachezaji makini katika kila eneo, wameamua kuboresha mikakati yao kuhakikisha kuwa wanafanikiwa kutwaa taji lolote msimu huu.

Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya Simba ni kwamba mabosi hao wameanzisha mpango maalum wa kutoa motisha kwa wachezaji wake ambapo imeanzisha utaratibu maalum wa kukusanya kiasi cha fedha ambacho inakitoa kama motisha kwa nyota hao pindi wanaposhinda mechi.

Simba msimu huu inakabiliwa na changamoto ya fedha kutokana na waliokuwa wadhamini wao kampuni ya bia TBL kujitoa lakini jambo hilo limewafanya mabosi wa timu hiyo kuamua kuanzisha utaratibu mpya wa kupata mkwanja ili nyota wake wasikose posho pindi wanapozikatili timu nyingine za Ligi Kuu kama walivyoifumua Ndanda FC ya Mtwara wikiendi iliyopita.

Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele alisema; “Msimu huu tuna malengo makubwa zadi hivyo tumekuja na mikakati mipya, hatutumii posho za mwaka jana maana hayo yalikuwa ni ya wakati mwingine na sasa ni nyakati nyingine.”

Kahemele ambaye amewahi kuwa kiongozi Azam alisema; “Mbali na kwamba hatuna wadhamini bado tuna uwezo mkubwa wa kupata fedha ambazo zinatosha kuwapa wachezaji pindi wanaposhinda mechi, siwezi kusema ni kiasi gani ila tumefanya maboresho. Tuna vyanzo mbalimbali vya mapato kwa ndani ambavyo vinatosha kabisa kukamilisha zoezi hilo. Wachezaji wanagawana kulingana na namna walivyocheza, waliovaa jezi wanapata posho kubwa zaidi ya wale ambao hawakuwa na nafasi, hii inaongeza ushindani ndani ya timu.”

Katika hatua nyingine, Kahemele alisema tayari wamewasilisha dokezo katika kampuni kadhaa kuomba udhamini na sasa mazungumzo yanaendelea kuona namna wanavyoweza kupata udhamini mkubwa zaidi ya ule wa Sh 500 milioni waliokuwa wakipata kutoka TBL.

“Kwanza udhamini wa TBL ulikuwa mdogo sana, nadhani sasa ni wakati muafaka kupata udhamini mkubwa zaidi, tayari tumepeleka proposal (dokezo) katika kampuni kadhaa na mazungumzo yanaendelea, pengine habari njema zitakuja hivi karibuni,” alifafanua.