Wachezaji 80 wataka kusajiliwa Njombe Mji

Mbeya.  Zaidi ya wachezaji 80 walioachwa na timu zao zinazoshiriki ligi mbalimbali nchini na nje ya nchi wamejitokeza kutaka kusajili wa Klabu ya Njombe Mji ya mkoani Njombe baada kutangaa kufanya usajili.

Njombe Mji imeanza kufanya majaribio ya wachezaji wiki hii, kwa lengo la kupata wachezaji 25, watakaosajili tayari kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

 Njombe Mji ni kati ya klabu tatu zilizopanda daraja msimu uliopita kutoka ligi daraja la kwanza ikiungana na Singida  United na Lipuli  FC ya Iringa.

 Katibu wa Njombe Mji, Widden Daphet 'Master' amesema idadi kubwa ya wachezaji wamejitokeza kufanya majaribio.

Alisema usaili huo unafanywa chini ya Kocha Mkuu Hassan Banyai  akisaidiwa na kocha msaidizi Mlage Kabange.

‘’Tunaangalia wachezaji wenye viwango bora wala hatutojali ametokea katika timu gani, lakini itategemea na ushauri wa kocha Banyai,’’ alisema.

Alisema ‘’Siyo kumalizika kwa zoezi hili ndiyo tutakuwa tunatangaza kikosi rasmi, hii ni hatua ya mwanzo tu na Mei 28 mwaka huu tutawashindanisha tena kwa mara ya pili ili sasa kuona nani yupo fiti na nani aachwe,’’alisema Daphet

‘’Hata hao wa Nigeria, Zambia na Malawi wanaokuja lazima wafanyiwe majaribio ili kuona je wao wana viwango kuliko watakaopata nafasi kwa sasa, tunataka kuwa na kikosi tishio,’’alisema.