Waarabu wanne waitaka Yanga

Muktasari:

  • Rais wa TFF, Jamal Malinzi, ametamka kuwa Yanga wanapewa kombe hilo moja kwa moja baada ya kulitwaa mara tatu mfululizo ambapo watakaa chini na wadhamini, Vodacom, kuona jinsi ya kutengeneza kombe jipya kwa ajili ya msimu ujao.

YANGA ikiipiga Mbao kesho Jumamosi jijini Mwanza itakuwa rasmi kwamba ni mabingwa wa Tanzania hata kama Simba itakuja kushinda rufaa yake iliyoko Fifa.

Lakini taarifa mpya ni kwamba timu nne ngumu za Uarabuni tayari zimeshafuzu Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao na zimekaa mkao wa kula kumsubiri yeyote atakayeanguka mikononi mwao.

Timu hizo ni Al Ahly ya Misri, Esperance na Etoile du Sahel zote za Tunisia pamoja na Wydad Casablanca ya Morocco.

Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limetangaza kwamba kama Yanga ikitawazwa rasmi mabingwa msimu huu, wao watalazimika kununua kombe jipya msimu ujao.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi, ametamka kuwa Yanga wanapewa kombe hilo moja kwa moja baada ya kulitwaa mara tatu mfululizo ambapo watakaa chini na wadhamini, Vodacom, kuona jinsi ya kutengeneza kombe jipya kwa ajili ya msimu ujao.

Ikumbukwe kwamba hii ni mara ya nne kwa Yanga kutwaa ubingwa mara tatu mfululizo tangu kuanzishwa kwa ligi mwaka 1965 wakati watani zao Simba wao wameweza kumiliki kombe hilo moja kwa moja mara moja pekee.

Kwa mara ya kwanza Yanga kubeba kombe hilo mara tatu mfululizo ilikuwa ni mwaka 1968 hadi 1970 na baadaye kushinda ubingwa mara mbili mfululizo kabla ya Simba nao kubinafsisha kombe hilo mwaka 1976 hadi 1978 na kushinda tena ubingwa mara tatu mfululizo. Yanga na Simba walipokezana ubingwa huo ikiwa na maana kwamba Yanga ilishinda miaka mitano mfululizo hivyo hivyo kwa Simba.

Yanga ilifanikiwa tena kutetea ubingwa mara tatu mfululizo mwaka 1991- 1993, 1996- 1998 na sasa mwaka 2014 - 2017 ambapo wamebakiza mechi moja pekee dhidi ya Mbao itakayochezwa kesho Jumamosi uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Pamoja na kwamba Simba imewahi kubaki na kombe moja kwa moja mara moja, lakini imewahi kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo kwa nyakati tofauti mwaka 1994 na 1995 huku Mtibwa Sugar nao wakibeba ndoo hiyo mara mbili mfululizo mwaka 199 na 2000 kabla ya Yanga nao kushinda kombe hilo mara mbili mfululizo kwa miaka minne tofatu. ilishinda mwaka 2005 na 2006 baadaye akatwaa ubingwa mwaka 2008 na 2009.

Akizungumza na Mwanaspoti, Malinzi alisema: “Yanga wanapewa kombe moja kwa moja maana wametwaa ubingwa huo mfululizo hivyo lazima kombe jipya litengenezwe na muundo utategemea na mapendekezo ya mdhamini kwa anahitaji kombe la aina gani, hivyo mazungumzo yatafanyika kati ya wadhamini na Bodi ya Ligi ndipo thamani itajulikana.”

NDOLANGA APIGWA BUTWAA

Mwenyekiti wa zamani wa FAT sasa TFF, Muhidin Ndolanga, ameweka wazi kwamba enzi za uongozi wake haijawahi tokea timu kuchukua ubingwa mara tatu mfululizo na kudai Yanga wameweka rekodi ya aina yake wakati huo huo,akitoa tahadhari.

“Haijawahi tokea timu kuchukua ubingwa mara tatu mfululizo, swali ni je Yanga kupata mafanikio hayo yamesaidia nini soka letu la Tanzania? Maana soka la bongo lina mambo mengi ndani yake na ndiyo maana hakuna tunapofika zaidi ya kuishia kutambiana na sifa ambazo hazina msaada,”alisema

Ndolanga, alieleza kwamba kuna haja ya kuchunguza ni kitu gani kimejificha katikati kinachofanya timu zisiwe na jipya kimataifa wakati zinashindanishwa na ligi ya ndani na bingwa anapatikana kwa halali.

“Tukihitaji kusonga mbele na Tanzania iwe na mafanikio lazima tunayochekelea yaendane na vitendo vya kuwa washindani kimataifa kwa kupeperusha vyema bendera ya taifa, hilo ndilo la msingi na msaada kwa  wachezaji wenye uwezo kupanua wigo wa ajira zao,”alisema

Kiongozi huyo alisema anaamini Tanzania ina vipaji vya soka vinavyoweza kuzaa matunda kimataifa huku akimtolea mfano Mbwana Samatta anayecheza Genk ya Ubeligiji, kwamba ameonyesha mfano kwamba inawezekana.

“Nasujudu soka la vijana ninaoamini wakijengewa misingi sahihi ndiyo watakaokomboa soka la Tanzania kutoka tulipo na kuanza kuheshimika kimataifa na pia kupata timu nzuri ya taifa,”alisema.