Verratti atamani taji Ligi ya Mabingwa

Monday March 6 2017

 

Paris. Kiungo wa Paris Saint-Germain, Marco Verratti amesema hana mpango wa kuondoka kwenye klabu hiyo.

Alisema matarajio yake ya kuendelea kuwapo kwenye klabu hiyo ni kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa akiwa nchini Ufaransa.

Awali, matarajio ya Verratti  ilikuwa ni kuendelea kutawala kwenye vichwa vya habari vinavyoripotiwa kutoka kwenye Ligi ya Serie A, kutokana na kuwapo wa miamba ya soka kama vile Juventus na Inter.

Mchezaji huyo mwenye miaka 24, aliyesajiliwa kwa mkataba wa miaka mitano tangu Agosti mwaka jana, alikuwa akizungumza mara kwa mara kuhusu uamuzi wake  wa kuachana na na PSG kabla ya kutengua kauli yake.

 “Ninahitaji kuendelea kuwepo hapa,” alisema Verratti ambaye timu yake ina kumbukumbu ya kuitungua Barcelona kwa mabao 4-0 wakati zilipokutana katika mchezo wa raundi ya kwanza jijini Paris.

Alisema, “Mimi ni sehemu ya mkatati wa ushindi. Ndoto yangu ni kushinda taji la Ligi ya Mabigwa nikiwa na PSG.”

Verratti aliongeza, “Ninamshukuru kocha kwa sababu amekuwa msaada kwangu na kunifanya niwe na ujasiri na ndiyo ilikuwa njia pekee ya kuyafikia mafanikio ninayoyataka.”

“Kwa sasa najisikia vyema na nina uwezo wa kucheza mechi hata tatu kwa wiki moja bila kupata tatizo la kiafya. Katika soka la kisasa jambo la muhimu ni kuwa na afya njema wakati wote.”