Ulaya yasaka vipaji vya filamu

Muktasari:

Shindano hilo linalotarajiwa kuendeshwa kwa wiki tatu litawahusisha vijana wenye umri kati ya 18 na 35 kutoka Tanzania Bara na Visiwani.

Dar es Salaam. Umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uholanzi, Ufaransa, taasisi ya Alliance Francaise pamoja na kituo cha British Council  wamezindua shindano la filamu kwa vijana (European Youth Film Competition).

Shindano hilo linalotarajiwa kuendeshwa kwa wiki tatu litawahusisha vijana wenye umri kati ya 18 na 35 kutoka Tanzania Bara na Visiwani.

Shindano hilo litaendeshwa chini ya kauli mbiu: ‘Ukuaji wa idadi ya watu: Je hii ni changamoto au fursa?

Mshindi wa shindano anatarajia kupata tuzo ya fedha taslimu Sh7 milioni, na mshindi wa pili Sh 5milioni na mshindi wa tatu atajinyakulia Sh3 milioni.

Kiongozi wa umoja huo nchini Tanzania, Balozi Roeland van de Geer  amesema  ‘kutokana na kasi kubwa ya ukuaji wa idadi ya watu hii inaleta changamoto pamoja na fursa katika shughuli za maendeleo.

“Kuongezeko kwa idadi ya watu tayari umeonesha  kuwa mzigo kwenye huduma za jamii kama afya, elimu, miundombinu na maeneo mengi kadhaa, lakini kwa upande mwingine ongezeko hilo linaleta rasilimali watu kwenye sekta nyingi za uzalishaji kutokan watu kuwa wabunifu na kwa hivyo kuleta ushindani katika utoaji huduma na uzalishaji,” alisema.

Alisaema shindano hili la filamu ni nafasi ya kipekee kwa vijana wa kitanzania kuonesha ubunifu wao kwenye eneo husika ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya Tanzania.

 

Shindano hili  litafanyika kwa awamu kabla mshindi hajapatikana. Awamu ya kwanza leo hadi Juni itahusu kupokea ingizo kwenye shindano, fomu za maombi zinapatikana. Alliance Francaise, British Council na Bodi ya Filamu Tanzania.

Washiriki 30 watachaguliwa kushiriki kwenye warsha ili kuwaelewesha kuhusu kanuni za utengenezaji wa filamu hizo pamoja  pamoja na kuwaelimsiha kuhusu dhana nzima ya ukuaji wa idadi ya watu nchini Tanzania.

Washiriki watatakiwa kutengeneza filamu fupu kati ya dakika 5 hadi 10. Majaji wtazingatia sana dhima, ubunifu, ubora wa picha pamoja na vigezo.