Ukiiga Yanga umekwisha

Muktasari:

Pointi hizo 15 za Yanga ni nyingi zaidi ya Liverpool yenye pointi 12 baada ya kucheza mechi nane na kumtimua aliyekuwa kocha wao mkuu, Brendan Rodgers.

ZAMANI kulikuwa na vituko sana. Unakumbuka yale magari yalikuwa chakavuuu... halafu yameandikwa kwa nyuma ‘Baba’ko analo?’. Mengi yalikuwa mbovu afu yalikuwa yanaegeshwa sehemu ya mteremko ili wakati wa kuondoka iwe rahisi kushtua hata lisipowaka.

Unaukumbuka ule msemo mwingine uliokuwa ukisema Iga Ufe? Basi ule unaihusu Yanga ya sasa, ukiwaiga tu umepotea. Angalia hapa. Imecheza mechi tano za Ligi Kuu Bara na kukusanya pointi 15 ambazo ni nyingi zaidi ya vigogo watatu wakubwa wa Ligi Kuu England ambao wamecheza mechi nane mpaka sasa.

Pointi hizo 15 za Yanga ni nyingi zaidi ya Liverpool yenye pointi 12 baada ya kucheza mechi nane na kumtimua aliyekuwa kocha wao mkuu, Brendan Rodgers.

Yanga pia imeiacha mbali Chelsea yenye pointi nane baada ya mechi nane wakati pia Tottenhan Hotspurs nayo ina pointi 13 baada ya idadi kama hiyo ya mechi. Hii inamaanisha kwamba endapo Yanga itashinda michezo mitatu ijayo itakuwa imewafunika mbali vigogo hao wa England ambao huwa hawakosekani katika tano bora.

Katika kuonyesha ujeuri wake, Yanga imezidiwa pointi moja pekee na Manchester United na Arsenal zenye pointi 16 kila moja wakati zikiwa zimecheza mechi tatu zaidi ya Yanga huku pia ikiwa sambamba na vigogo wa Hispania, Real Madrid na Barcelona wenye pointi 15 pia baada ya mechi saba.

Jeuri ya mabao

Kasi ya mabao ya Yanga msimu huu inaonekana kuzitoa nishai timu zote za Ligi Kuu na sasa imebainika kuwa timu sita zinazoshika nafasi za chini kwenye msimamo wa Ligi zikijumlisha mabao yake yote ndiyo yanafikia idadi ya mabao hayo ya Yanga.

Yanga imefunga mabao 13 katika mechi tano, mabao ambayo Ndanda ya Mtwara, Kagera Sugar, Mbeya City, African Sports, Coastal Union na JKT Ruvu kwa pamoja ndiyo yanafikia idadi hiyo.

Ndanda mpaka sasa ina mabao manne, Mbeya City matano, Kagera mawili wakati JKT Ruvu na African Sports zimefunga bao moja moja mpaka sasa huku Coastal Union ikiwa haina bao lolote.

Yanga pia imefunga mabao sita zaidi ya watani wao, Simba ambao wana mabao saba pekee katika mechi tano walizocheza.

Ukuta wa chuma

Yanga inakimbiza pia katika safu yake ya ulinzi na imefungwa bao moja pekee mpaka sasa wakati watani wao Simba tayari wameruhusu mabao matatu. Yanga ilifungwa bao hilo na beki wa JKT Ruvu, Michael Aidan.

Kikosi cha Yanga msimu huu kimekumbwa na mabadiliko kidogo katika safu yake ya ulinzi na Oscar Joshua amempisha Mwinyi Haji katika beki ya kushoto na Mbuyu Twite amecheza mechi zote tano kama beki wa kulia nafasi ambayo ilikuwa chini ya Juma Abdul msimu uliopita.

Azam na Mwadui nazo zinaonekana kukomaa na Yanga kwani katika mechi zao zimeruhusu mabao mawili pekee. Mwadui imefungwa mabao hayo mawili dhidi ya Toto Africans na Azam pekee katika mechi sita ilizocheza. Azam iliruhusu mabao hayo mawili dhidi ya Prisons na Mbeya City.

Kiiza awapiku mastraika 16

Wakati Yanga ikitamba kukimbiza vigogo na kuzidi timu za Ligi Kuu kwa mabao, Simba inajivunia uwepo wa straika wake, Amissi Kiiza ambaye mabao yake matano aliyofunga msimu huu ni zaidi ya mabao yaliyofungwa na JKT Ruvu, Coastal Union, African Sports na Kagera Sugar kwa pamoja ambazo zimefunga mabao manne.

Timu hizo nne zina mastraika 16 ambao kwa jumla yao wameshindwa kufunga mabao matano mpaka sasa. Mastraika wanaotamba na timu hizo ni pamoja na Gaudence Mwaikimba, Samweli Kamuntu na Saady Kipanga wa JKT Ruvu, Ali Shiboli, Bright Ike na Abaslim Chidiebele wa Coastal Union ambao hawajafunga bao hata moja mpaka sasa.

Maguli king’ang’anizi

Yanga ina wafungaji wake wawili katika orodha ya wafungaji watano wenye mabao mengi mpaka sasa lakini imebainika kuwa straika, Elius Maguli ndiye nyota mzawa pekee katika orodha hiyo iliyotawaliwa na wachezaji wa kigeni.

Orodha hiyo inaongozwa na Hamis Kiiza mwenye mabao matano, Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Maguli wenye mabao manne kila mmoja wakati Kipre Tchetche ni wa tano na mabao yake matatu.

Maguli amekuwa akifanya vizuri na Stand United msimu huu baada ya kuvunja mkataba wake na Simba na kujiunga na timu hiyo ya Shinyanga. Nyota huyo aliwahi kumaliza kama mpachika mabao wa pili kwenye msimu wa 2013/14 na alifunga mabao 14 akizidiwa mabao matano na Amissi Tambwe aliyeibuka kinara kwa mabao 19.

Coastal Union aibu

Licha ya kuwa na kocha bora, Jackson Mayanja, Coastal Union inaonekana kuwa katika wakati mgumu baada ya kushindwa kufunga bao lolote katika mechi sita ilizocheza msimu huu.

Coastal imetoka suluhu tatu dhidi ya Ndanda, Mwadui na Mgambo JKT na kupoteza michezo yake mitatu mingine. Timu hiyo ya Tanga ilisajili mastraika wanaoaminika kuwa wazuri akiwemo Shiboli na Chidiebele.