Tuwafunge tano kwani wao Arsenal au Wacomoro?

LAUDIT MAVUGO

Muktasari:

  • Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana Februari 25 katika pambano la marudiano la Ligi Kuu Kuu Bara.

STRAIKA Laudit Mavugo ambaye Simba walikuwa wakimkejeli kwamba ni garasa na hana lolote, jana Alhamisi amefunga bao pekee dhidi ya African Lyon Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Siyo bao tu, ushindi huo umeipeleka Simba kwenye robo fainali ya Kombe la FA na imekuwa timu ya kwanza kufuzu msimu huu. Bao hilo pia linamaanisha kuwa Simba imeanza kusikia harufu ya ushiriki wa michuano ya kimataifa mwakani.

Hilo lilikuwa bao la kwanza kwa Mavugo katika Kombe la FA ambalo liliwafanya mashabiki wa Yanga waliokuwa wakiishangilia Lyon wawaambie Simba wapige tano kama wao walivyofanya Comoro kwenye michuano ya kimataifa au Arsenal ilivyopigwa na Bayern. Lakini Simba wakawajibu kwa bango lililoandikwa ; “Tano za nini, kwani wao Wacomoro?”

Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana Februari 25 katika pambano la marudiano la Ligi Kuu Kuu Bara.

Bao hilo la Mavugo, limeisaidia Simba kulipa kisasi cha kipigo cha 1-0 ilichopewa na Lyon katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa mwishoni mwa mwaka jana lakini vilevile kumziba mdomo kipa Mkameruni wa Lyon, Youthe Rostand ambaye alikuwa akijinasibu kwamba Simba haimfanyi lolote.

Mavugo alifunga bao hilo dakika ya 58 akimalizia pasi murua ya Ibrahim Ajib aliyepiga mpira huku kipa wa Lyon, Rostand akiwa chini baada ya kuteleza na kuanguka.

Simba walikuwa na uwezo wa kuondoka na karamu ya mabao kama sio umakini mdogo wa mastraika wake kuwaangusha kwa kupiga mashuti yaliyokuwa akiishia mikononi mwa kipa Rostand au kupanguliwa nje.

Dakika ya 13, Said Ndemla alitingisha lango la wapinzani kwa kupiga shuti kali ambalo liliokolewa na Rostand ambapo Juma Liuzio naye alipiga shuti dakika ya 17 lakini kwa umakini, kipa wa Lyon aliweza kulipangua shuti hilo.

Hata hivyo, Ajib ambaye alikuwa katika nafasi nzuri ya kuipatia timu yake bao alijikuta anapiga shuti lisilokuwa na madhara kwa wapinzani wao ikiwa ni dakika ya 27 huku Mavugo akifanyiwa faulo na mchezaji wa Lyon ambapo mwamuzi Ludovic Charles aliamuru ipigwe faulo fupi aliyopiga Ajib lakini iliokolewa na wachezaji wa Lyon.

Jonas Mkude alipokea pasi ya Ndemla dakika ya 35 akiwa karibu na eneo la katikati ya uwanjani ambapo alipiga shuti ndefu iliyotua mikononi mwa Rostand ambaye alionekana kuwa na umakini mkubwa.

Kocha wa Lyon, Charles Otieno alifanya mabadiliko ya mpigo kwa kuwatoa Hamad Manzi aliyeumia, Rehani Kibindu, Omary Daga nafasi zao zilichukuliwa na Awadh Juma, Fred Cosmas na Abdallah Mguye huku Joseph Omog akiwatoa Juma Liuzio, Ndemla na Mavugo na kuwaingiza Shiza Kichuya, Mohamed Ibrahim na Pastory Athanas.

Mwamuzi alitoa kadi za njano kwa Hamad Waziri dakika ya 53 kwa kuchelewa kupiga mpira, Rostand naye akizawadiwa kadi dakika ya 55 kwa kudakia mpira nje ya eneo pamoja na Adam Miraji aliyepewa kadi ya njano dakika ya 62.

Wakati huo huo, kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka leo Ijumaa asubuhi kwa boti kuelekea Zanzibar ikiwa ni maandalizi ya mechi yao ya Ligi Kuu Bara dhidi ya mahasimu wao Yanga ambayo itachezwa Februari 25 mwaka huu.