Timu 54 kusaka Sh 10milioni kikapu

Dar es Salaam.Timu 54 zimejitokeza kushiriki mashindano ya mpira wa kikapu ya EATV B-Balls  bingwa ataondoka na kitita cha Sh 10 Milioni.

Mashindano hayo yataanza kutimua vumbi Juni 3 jijini Dar es Salaam ambapo yatafanyika kwa mtindo wa mtoano.

Ofisa Masoko wa EATV, Basilisa Biseko, alisema timu 54 zitashiriki katika mtoano ili kupata zitakazoingia hatua ya 16 bora, robo fainali mpaka fainali.

"Kila timu itakuwa na wachezaji 10 na atakayefungwa anaondoka hadi nusu fainali kabla ya mchezo wa fainali," aliongeza.

Akizungumzia hamasa ya timu katika kujitokeza kushiriki mashindano hayo, Biseko alisema haijawahi kutokea ukizingatia ndiyo mara ya kwanza yanafanyika.

"Tunaamini mashindano yatakuwa yenye msisimko hasa kutokana na muitikio wa watu na pia hamasa ya wacezaji wakati wa usajili ni wazi wamepania,".

EATV B-balls yamedhaminiwa na Kampuni ya Coca Cola kupitia kinywaji chake cha Sprite huku Shirikisho la mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) linashirikiana na EATV yakishirikiana kuratibu ambapo mbali na zawadi kwa bingwa pia mshindi wa pili na mchezaji bora watazawadiwa.