Tambwe apima makali ya Mavugo

FOWADI Mrundi Amissi Tambwe amecheza nchini kwa miaka mitatu na kufunga mabao 54 kwenye Ligi Kuu Bara tu na kuweka rekodi kadhaa ikiwemo ya kufunga ‘hatrick’ sita lakini imebainika kuwa rekodi kadhaa zilizomshinda sasa zinatazamiwa kuvunjwa na Mrundi mwenzie, Laudit Mavugo aliyetua Simba.

Mavugo ametua Simba kwa mbwembwe ambapo usajili wake kwa jumla umeigharimu klabu hiyo zaidi ya Sh 120 milioni na sasa rekodi kadhaa zilizomshinda mtangulizi wake huyo zinamkabili. Staa huyo tayari amefunga bao moja katika mechi moja ya ligi kuu aliyocheza.

Kwanza, Mavugo ambaye kwa misimu miwili pale Burundi amefunga mabao zaidi ya 60, anakabiliwa na kazi ngumu ya kufunga mabao matatu ‘hatrick’ kwenye mechi moja ya watani wa jadi, Simba na Yanga ili kuvunja rekodi ya Abdallah Kibadeni iliyodumu kwa miaka 39 sasa. Kibadeni alifunga mabao hayo matatu mwaka 1977 wakati Simba ilipoifunga Yanga kwa mabao 6-0.

Straika huyo mwenye vitu vingi uwanjani anakabiliwa na kazi ya pili ambayo ni kuvunja rekodi ya mabao mengi kwenye msimu mmoja iliyowekwa na Mohammed Hussein kwa kufunga mabao 26 kabla ya baadaye kukaribiwa na Abdallah Juma aliyefunga mabao 25. Rekodi hizi mbili zimemshinda Tambwe mpaka sasa.

Mavugo atalazimika pia kutumia nguvu nyingi kuvunja rekodi ya Edibily Lunyamila ya kufunga mabao mengi katika mchezo mmoja aliyoweka kwenye mchezo dhidi ya RTC Kagera ambapo alifunga mabao sita Yanga iliposhinda kwa mabao 8-0. Tambwe amewahi kufunga mabao manne kwenye mchezo mmoja lakini ameshindwa kufikia sita ya Lunyamila.

Katika hatua nyingine Mavugo anakabiliwa na mtihani wakuvunja pia rekodi ya ‘hatrick’ mbili kwa msimu iliyowekwa na Tambwe ambaye amefanya hivyo kwa misimu mitatu mfululizo na kufikisha hatrick sita.

MKWASA ANENA

Kocha wa Taifa Stars, Boniface Mkwasa alisema tatizo kubwa ambalo linawakabili mastraika wa sasa hadi kushindwa kuvunja rekodi hizo za kipindi cha nyuma ni mitazamo yao katika soka pamoja na mabadiliko ya mazingira.

“Unajua kwa sasa ni vigumu kuweza kupata straika mwenye mitazamo kama ya ilivyokuwa kwa wachezaji wa zamani, hata kama atakuwa mzuri bado atakuwa anapungukiwa baadhi ya vitu, hii ndiyo maana leo duniani tunaona wachezaji wengi wazuri lakini ni vigumu kupata mchezaji kama Pele,” alisema Mkwasa.

“Mazingira pia yamebadilika, zamani kidogo kuna kipindi ushindani haukuwa mkubwa sana kama ilivyo sasa, yawezakana pia hili nalo linachangia kwani kupata timu dhaifu ya kufanya hivyo inakuwa shida.

“Mfano kuna baadhi ya mechi kipindi cha nyuma ungeweza kukuta mchezaji anacheza huku anawaza mapato ya mlangoni hivyo akili inakuwa haipo uwanjani, kumfunga mtu huyu mabao mengi siyo jambo gumu sana, kwa sasa mazingira hayapo hivyo,” alifafanua kocha huyo wa zamani wa Yanga.