Takukuru wakomalia wakubwa TFF

Muktasari:

Chacha na Matandika waliokuwa wakikabiliwa na shtaka la kuomba rushwa ya Sh25 milioni waliachiwa huru na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma  Shaidi baada ya kuwaona hawana kesi ya kujibu.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imewasilisha kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi ya uamuzi uliowaacha huru vigogo wawili wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Martin Chacha na Juma Matandika.

Chacha na Matandika waliokuwa wakikabiliwa na shtaka la kuomba rushwa ya Sh25 milioni waliachiwa huru na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma  Shaidi baada ya kuwaona hawana kesi ya kujibu.

Mbali na kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa mahakamani hapo, Takukuru pia wanaomba kupewa nakala za mwenendo wa kesi hiyo na ya uamuzi huo uliowaachia huru.

Hakimu Shaidi aliwaachia huru washtakiwa hao baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi saba wa upande wa mashtaka na kuona upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shtaka pasipo kuacha shaka.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Shaidi alisema katika ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka unaonyesha hakuna mtu aliyelalamika zaidi ya sauti kusambaa katika simu na mitandao.

Alisema ushahidi wa mashahidi saba wa upande wa mashtaka haukuonyesha je ni kweli walienda TFF ama la, wala hakukuwa na uthibitisho ni kweli walitoka Geita kuja Dar es Saalam.

Kuhusu sauti zilizotambuliwa za Martin na Juma kupitia CD, Hakimu Shaidi alisema watu wana sauti za kufanana na hata kuigizana ni hatari tukiegemea huko hivyo ni lazima pawepo na uthibitisho.

Sakata hilo linadaiwa kutokana na rufaa iliyokatwa na Panone FC ya mkoani Kilimanjaro na Rhino Rangers dhidi ya Polisi Tabora kwa kumchezesha mchezaji ambaye anadaiwa kuwa si raia wa Tanzania, Seleman Jingu.

Washtakiwa hao, wanadaiwa kufanya kosa hilo Februari 4,2016, ambapo wakiwa waajiriwa wa TFF waliomba rushwa ya Sh25 milioni kutoka kwa Salum Kulunge na Constantine Morandi ambao ni maofisa kutoka Chama cha Soka cha Geita na Klabu ya Geita Gold Sports ambayo ilishushwa daraja sambamba na Polisi Tabora, Kanembwa JKT na Oljoro JKT kwa tuhuma za upangaji matokeo ya Ligi Daraja la Kwanza misimu uliopita.