TPLB, TFF ni zaidi ya jipu soka la Tanzania

Muktasari:

Mwanaspoti ni kama ilivyo kwa vyombo vingine vya habari nchini ni kisemeo cha wananchi. Ni kipaza sauti cha wadau wa michezo ikiwamo soka, moja ya michezo inayopendwa na kuwanufaisha wengi ndani na nje ya nchi.

HATUTAACHA kusema, kukemea na kushauri kwa lolote litakalokuwa likitokea ama kufanywa ndani ya Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ujumla, hata kama viongozi wake wanapuuza tunachokisema mara kwa mara. Mwanaspoti ni kama ilivyo kwa vyombo vingine vya habari nchini ni kisemeo cha wananchi. Ni kipaza sauti cha wadau wa michezo ikiwamo soka, moja ya michezo inayopendwa na kuwanufaisha wengi ndani na nje ya nchi. Inawezekana viongozi wa vyombo hivyo viwili na Kamati ya Mashindano ya TFF zinafanya kusudi na kutaka kuonyesha kuwa, hata wanangwe vipi katu hawawezi kubadilika na hakuna wa kuwagusa kwenye maamuzi yao. Ni kweli hata Mwanaspoti halina nguvu ya kuwa mabosi wa TFF wala TPLB, ila tuna wajibu mkubwa wa kuyasema yale yote ambayo yanafanyika ndani ya vyombo hivyo, iwe ni mazuri ama mabaya, ilimradi kuona soka letu linasimama kwenye mstari. TPLB na TFF kwa ujumla imekuwa na kiburi katika suala zima la panga pangua ya ratiba ya Ligi Kuu Bara, bila kujua kama mara nyingi maamuzi hayo ya kubadilishwa kwa ratiba kila uchao huziumiza na kuziathiri klabu zisizojiweza pamoja na mashabiki wa soka. Klabu zenye uchumi mdogo zimekuwa wahanga wa maamuzi hayo ya kibabaishaji yanayofanywa kila mara na vyombo hivyo na watendaji wa TFF.

Ni kweli Rais wa TFF, Jamal Malinzi na hata watendaji wake walishawahi kutoa misimamo yao kwamba, mabadiliko ya ratiba ya Ligi Kuu hayakwepeki kwa vile kuna sababu mbalimbali za msingi.

Lakini, ukweli ni kwamba kuna wakati mabadiliko hayo yanafanyika na kuweza hata kutamka huwa yanalenga kuzibeba timu kubwa na kuzitengenezea mazingira ya kubeba ubingwa ama kufanya vizuri katika ligi hiyo. Kwa mfano jana Ijumaa Yanga na Stand United zilikuwa uwanjani kucheza, katika mechi ambayo awali ilikuwa ichezwe kesho Jumapili. Maamuzi hayo yanaweza kuonekana kuwashtukiza klabu zote mbili, lakini ukweli Yanga wananufaika zaidi kwa sababu wapo nyumbani tofauti na Stand waliokuja na uchovu wa safari kutoka Tanga. Pia ratiba iliyowahi kutolewa mapema na TFF ilikuwa ikionyesha hivyo, lakini ghafla ikabadilishwa huku hata klabu zikiwa hazina taarifa na kukiwa hakuna sababu za maana. Katika ratiba iliyosambazwa na Afisa Habari wa TFF, Alfred Lucas juzi Alhamisi inaonyesha kuwa mechi ya Azam na Ndanda inapaswa kuchezwa leo Jumamosi, lakini maelezo yaliyoambatana na ratiba hiyo inaeleza itachezwa kesho Jumapili, huku Azam wenyewe wakijua itapigwa Jumanne. Sio hiyo tu haya Mbeya City na JKT Ruvu wanajua wanacheza kesho Jumapili, lakini ratiba inawaeleza watacheza leo Jumamosi. Huu ni mkanganyiko wa ajabu kabisa kwenye Ligi yetu.

Kadhalika inaelezwa kuwa wikiendi ijayo itakayohusisha Februari 10-12 hakutakuwa na mechi zozote za Ligi Kuu tofauti na ratiba inavyoonekana kuwa kuna mechi zaidi ya tano, kisingizio ni kuwepo kwa pambano la kimataifa la Yanga. Yanga inaenda Comoro kucheza na Ngaya de Mbe na ni wawakilishi hao tu ndio wenye mchezo, hivyo pambano lao dhidi ya Ruvu Shooting likiahirishwa ni sawa, vipi kwa mechi za timu nyingine ambazo hazina majukumu ya kimataifa? Hii ni aibu kubwa kwa TPLB, TFF na hata Malinzi kama Rais wa shirikisho hilo. Ni kama kazi imemshinda ama watendaji aliowapa kazi wanamuangusha na yeye amekubali kunyamazia upuuzi huo kulinda cheo chake. Imefika wakati TFF na Bodi ya Ligi zikajisikia aibu na kuepukana na lawama za kila mara wanazopewa na kuishia kuona kama wanaosakamwa. Haya wanayataka wenyewe kwa sababu ya kuendesha mambo kibabaishaji mno.

Kuna sababu za msingi za kubadilisha ratiba kama ilivyotokea muingiliano wa mechi ya kimataifa, lakini bado TFF na TPLB zilipaswa kuzichunguilia kwa kina kalenda za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na lile la Dunia (FIFA) ili kuepuka kuonekana kama wapuuzi wanaoendesha mambo kwa mtindo wa bora liende. Mwanaspoti linadhani pia kuna tatizo kubwa ndani ya TFF hasa idara ya Habari na Mawasiliano katika usambazaji wa taarifa zao juu ya mambo yanayofanyika ndani ya shirikisho hilo zikiwamo ratiba za michuano mbalimbali. Sio katika Ligi Kuu Bara, bali hata ligi nyingine na michuano ya Kombe la FA, mambo yanaonekana kuendeshwa kwa mtindo wa kukurupuka ambayo ni kati ya yanayofanya mechi za soka kupoteza mvuto na msisimko kwa mashabiki.Ratiba zinabadilishwa ghafla, bila taarifa kwa mashabiki ambao ndio wanaoenda uwanjani, idara ya masoko na uenezi TFF inafanya kazi gani? Imefika wakati mabosi wa idara hizo na TFF kwa ujumla kubadilika, ili kuepuka aibu hii na mzigo wa lawama wa kila mara.