TFF ijue namna ya kuheshimu ratiba yake

Muktasari:

JUZI, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza ratiba ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) Tanzania Bara msimu wa 2015/16.

JUZI, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza ratiba ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) Tanzania Bara msimu wa 2015/16.

Kama ilivyo ada kwa soka la Tanzania inapotangazwa ratiba, mashabiki wa soka huwa na shauku ya kujua timu mahasimu za Yanga na Simba zinakutana lini.

Licha ya kwamba ligi hiyo inatarajiwa kuanza Agosti 20 mwaka huu lakini habari kubwa kwa mashabiki wa soka ilikuwa ni Oktoba Mosi, siku ambayo mahasimu hao wa jadi katika soka watakapoonyeshana umwamba, Uwanja wa Taifa.

Maoni mbalimbali yameanza kutolewa kuhusu ratiba hiyo, wapo ambao wameanza kuikosoa lakini pia wapo tena wengi tu ambao wameonekana kuiunga mkono kwa sababu mbalimbali.

Tusingependa kuingilia suala la ubora au udhaifu wa ratiba hiyo tukiamini jambo hilo linahitaji tafakuri ya kina ambayo inaweza kutolewa kwa mapana na viongozi wa klabu husika za ligi.

Jambo la muhimu ambalo tungependa kulizungumza hii leo ni umuhimu wa TFF kuiheshimu ratiba hii ambayo kimsingi ni yao na wanajua waliyoyazingatia wakati wakiiandaa.

TFF pamoja na Bodi ya Ligi, ndio wenye ratiba hii na hivyo sifa zote na mapungufu yatawahusu moja kwa moja.

Sote tunakumbuka namna ambavyo ratiba ya ligi msimu uliopita ilivyopanguliwa bila sababu za msingi lakini kubwa ambalo limeendelea kuwa katika kumbukumbu ni kitendo cha TFF kuiruhusu Azam kwenda Zambia wakati ligi ikiendelea.

Uamuzi huo wa TFF ambao ulisababisha Azam kuwa na viporo ulilalamikiwa na wadau wengi wa soka kiasi cha kujenga dhana kwamba ulikuwa mkakati wa kuibeba timu hiyo.

Na ingawa Rais wa TFF, Jamal Malinzi alikiri kosa hilo lakini bado kwa wadau imekuwa vigumu kuwafanya wakubali kirahisi kwani imani ya wengi ni kwamba TFF kama taasisi ina watu ambao walihusika katika uzembe huo na walipaswa kuadhibiwa.

Kwa upande wetu tunasema yaliyopita yamepita, tunachotaka sasa ni kuiona TFF ikiwa katika mstari, ikijitoa katika lawama za kuvuruga ratiba ambayo ni mali yao.

TFF ihakikishe ratiba hii inaanza na kufikia hapo itakapofikia na kama kuna mabadiliko basi mabadiliko hayo yafanyike kwa kuzingatia mambo ya ulazima tena yaliyo nje ya uwezo wa mwanadamu kama mvua, mafuriko na mengineyo.

Tutashangaa kama itatokea kwa TFF kuahirisha baadhi ya mechi zilizopangwa katika ratiba yao kwa sababu ambazo hazina msingi ikiwamo hiyo ya kuiruhusu timu kwenda kushiriki mashindano nje ya nchi.

TFF itajijengea heshima yake iwapo itakuwa tayari kusimamia ratiba hiyo na kutokuwa tayari kuyumbishwa na mambo yasiyo na ulazima kama ambavyo imejitokeza msimu uliopita.

Kurudia kwa mara nyingine kosa hilo au linalofanana na hilo kutawafanya wadau wa soka nchini waamini kuwa TFF ama inatumika au ina viongozi wazembe wasioheshimu mambo ya msingi.

Ni vyema TFF wakadhamiria kuifanya ratiba hii iwe kipimo cha utendaji wao katika umakini na kuheshimu maamuzi yao.