TFF ijikite kuitangaza Ligi ya Vijana

Rais wa TFF, Jamal Malinzi

Muktasari:

Kwa upande wa Bukoba Azam U-20 ndiyo inaongoza ligi hiyo ambayo jana ilifikia tamati wakati kwa upande wa Dar es Salaam Simba ndiyo ilikuwa kidedea. Hatua hiyo ya makundi imekwisha sasa na itafuatia hatua ya nne bora ambapo timu zitacheza kwa mfumo wa ligi na timu itakayokusanya pointi nyingi ndiyo itakuwa bingwa.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) ndiyo lenye dhamana na Ligi ya Vijana ambayo inaendelea katika mikoa ya Dar es Salaam na Kagera ikishirikisha timu 16 za vijana chini ya miaka 20 ambazo zinatokana na zile zinazoshiriki Ligi Kuu.

Kwa upande wa Bukoba Azam U-20 ndiyo inaongoza ligi hiyo ambayo jana ilifikia tamati wakati kwa upande wa Dar es Salaam Simba ndiyo ilikuwa kidedea. Hatua hiyo ya makundi imekwisha sasa na itafuatia hatua ya nne bora ambapo timu zitacheza kwa mfumo wa ligi na timu itakayokusanya pointi nyingi ndiyo itakuwa bingwa.

Hata hivyo, pamoja na kuanzisha ligi hiyo na kufanikisha kufanyika kwake kwa mara ya kwanza mwaka huu ikichukua njia ya yale mashindano ya kombe la Uhai yaliyofanyika kwa mara ya mwisho mwaka 2013, bado msisimko umekuwa mdogo tofauti na ilivyotarajiwa.

Ikumbukwe kuwa kipindi cha nyuma michuano hiyo ilipokuwa ikifahamika kama Kombe la Uhai ilikuwa na msisimko mkubwa na mvuto zaidi tofauti na sasa ambapo licha ya kuonyeshwa moja kwa moja kupitia Azam TV bado msisimko wake umekuwa chini.

Ukitazama ligi hiyo mpaka sasa haina mdhamini tofauti na Azam TV ambayo imenunua haki za matangazo ya televisheni hivyo zilihitajika jitihada za makusudi ili kuifanya ligi hiyo ijitangaze na kuvutia wadhamini mbalimbali ambao wangeweza kuwekeza.

Mfano mpaka sasa ni watu wachache ambao wanafahamu kama ligi hiyo imefikia hatua ya mwisho ya makundi na inaingia hatua ya nne bora ambapo timu shiriki sasa zitapambana kupata bingwa. Kama unafahamu basi umekuwa mfuatiliaji wa karibu kupitia Azam TV na si vinginevyo.

Tunaamini kuwa TFF ilitakiwa kuitangaza ligi hiyo na kuhakikisha inapata nafasi ya kusikika katika maeneo mbalimbali nchini na siyo kuiachia tu Azam TV ambayo inaonyesha tu mechi hizo na ikishamaliza inakuwa mwisho.

Ifahamike kuwa bila kuwekeza huwezi kupata wadhamini, hivyo TFF bado ina kazi kubwa ya kufanya katika hilo vinginevyo itaziacha timu hizo zikikumbwa na ukata mkubwa.

Kitengo cha habari cha TFF kilitakiwa kuufahamisha umma wa Tanzania juu ya ligi hiyo kwa kutoa taarifa za maendeleo yake kwa kushirikiana na Azam jambo ambalo lingeweza kuwavuta wawekezaji kuingia na kudhamini ligi hiyo.

Ifahamike tu kuwa kampuni ambazo zimekuwa zikitaka kuwekeza katika soka zimekuwa zikitaka kupata uhakika wa kupata wasaa wa kuonekana katika vyombo vya habari na kuwafikia watu wengi zaidi.

Wakati huu ambapo Ligi Kuu Bara imesimama na hakuna michuano mikubwa yoyote inayoendelea nchini, ingekuwa ni sehemu mwafaka wa kuifanya ligi hiyo kuwa maarufu zaidi.

Jitihada hizo zingeweza kufanyika pia katika Ligi ya Wanawake na hatua za awali za Kombe la FA.

Ifike mahali TFF iache kufanya kazi kwa mazoea na kuona kuwa hii ni fursa ya kibiashara na ambayo ingeweza kuzivutia kampuni kadhaa kujitangaza kibiashara. Kama hutangazi ligi yako ni nani ataifahamu?

Miaka mitatu iliyopita wakati Kombe la Uhai likifanyika msisimko ulikuwa ni mkubwa kutokana na TFF ya kipindi kile chini ya Leodger Tenga kuifanya ligi hiyo kusikika na kufahamika zaidi.

Kila mtu alipenda kufahamu kuhusu kombe hilo ambalo bingwa wake mtetezi alikuwa Coastal Union ya Tanga.

Changamoto nyingine ikiwemo za umri inabidi zifanyiwe kazi katika mashindano yatakayokuja ili kuondoa utata kwani kumekuwa na malalamiko kadhaa juu ya uwezekano wa baadhi ya wachezaji kuwa na umri zaidi ya miaka 20.

Ikumbukwe kwamba suala la kudanganya umri ni kitu kibaya katika maendeleo ya soka la nchi yoyote ile.

Kwa mfano mtu anaweza kuwa na miaka 28 halafu akataja kwamba ana umri wa chini ya miaka 20, mtu kama huyo atacheza leo kwa ufanisi na pengine kusaidia kuipa timu yake kombe, lakini ni nani ataangalia kwa makini kesho ya mchezaji huyo au kuangalia kwa undani mwelekeo wa soka wa taifa hili.

Kama hakutakuwa na usawa katika ligi hiyo hata wadhamini watakuwa na woga kwani wataona wanajihusisha katika kitu ambacho kimejaa magumashi na mwisho wake wataonekana hata wao hawafai katika bidhaa au shughuli wanayoitangaza. Mwanaspoti linawakumbusha viongozi wa Shirikisho la Soka nchini kutafakari kwa makini na kuanza kuchukua hatua mapema.