Straika wa maana akwama Singida United

Muktasari:

Timu hiyo iliyopanda Ligi Kuu Bara kwa ajili ya msimu ujao, ilifanya mazungumzo na straika huyo wa nguvu kwa ajili ya kuimarisha safu yake ya ushambuliaji, lakini iliposikia dau lake tu ikaleta hadithi ya sizitaki mbichi hizi.

SINGIDA United imeanza kutishia ufalme wa klabu kongwe nchini kwa namna inavyofanya usajili wa nyota wa kigeni kwa fujo, lakini kwa Mnyarwanda Danny Usengimana, imekwama kutokana na dau kubwa analolitaka.

Timu hiyo iliyopanda Ligi Kuu Bara kwa ajili ya msimu ujao, ilifanya mazungumzo na straika huyo wa nguvu kwa ajili ya kuimarisha safu yake ya ushambuliaji, lakini iliposikia dau lake tu ikaleta hadithi ya sizitaki mbichi hizi.

Straika huyo wa Polisi Rwanda mwenye mabao 15 mpaka sasa katika mechi 23 za Ligi Kuu Rwanda, klabu yake imetaja dau lake ambalo limewafanya mabosi wa Singida United kurudi nyuma kidogo.

Kwa mujibu wa gazeti la The News Times la nchini Rwanda, dau la kumng’oa Usengimana kwenye kikosi cha Polisi ni Faranga 8 milioni za Rwanda ambazo ni sawa na Dola 100,000 (zaidi ya Sh210 milioni) fedha ambazo ni sawa na zile Yanga ilizotumia kumsajili mshambuliaji Obrey Chirwa.

Gazeti hilo limefichua kuwa katika dau hilo, Usengimana mwenyewe angevuta kiasi cha Dola 40,000 ( zaidi ya Sh80 milioni) huku kiasi kilichobakia kikienda kwa timu yake.

Sasa wakati straika huyo akifunguka kuwa ameshamalizana kila kitu na Singida United, mabosi wa timu hiyo wamemruka kimanga na kudai hayuko kwenye mipango yao.

“Ni taarifa tu ambazo vyombo vya habari vinaeneza, lakini kiukweli sisi hatujafanya usajili wa mshambuliaji huyo wala kuzungumza naye kama ambavyo inasemwa,” alisema Katibu Mkuu wa Singida, Abdulrahman Sima ikiwa ni kauli inayotofautiana na taarifa ya awali kuwa walikuwa wakimvizia.

“Jukumu la usajili ndani ya Singida lipo mikononi mwa Kocha Hans Pluijm ambaye kesho (leo) Alhamisi atakutana na uongozi kuweka mikakati yake ya kuimarisha kikosi ambacho kimesajili nyota watatu tu wa kigeni wote kutoka Zimbabwe.”

Mwanzoni mwa wiki hii, mshambuliaji huyo alinukuliwa na gazeti moja la Rwanda akisema anachongojea kwa sasa ni kumwaga wino tu kwenye fomu za usajili za Singida United.