Soka la Bongo aibu tupu

Muktasari:

Kagera ilipokwa ushindi wake wa mabao 2-1 iliyoupata kwenye pambano la Ligi Kuu Bara lililochezwa Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba dhidi ya Simba baada ya Simba kulalamika walimchezesha Fakih akiwa na kadi tatu za njano.

SAKATA la beki Mohammed Fakih limemalizwa rasmi juzi baada ya Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji chini ya Mwenyekiti wake Richard Sinamtwa kutoa maamuzi ya kuirudishia Kagera Sugar ushindi wao wa awali.

Kagera ilipokwa ushindi wake wa mabao 2-1 iliyoupata kwenye pambano la Ligi Kuu Bara lililochezwa Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba dhidi ya Simba baada ya Simba kulalamika walimchezesha Fakih akiwa na kadi tatu za njano.

Kamati ya Saa 72 iliyapitia malalamiko ya Simba na kutoa maamuzi ya kuipa timu hiyo ushindi wa pointi na mabao matatu baada ya kuridhika na ushahidi waliopelekewa kabla ya Kagera kuomba marejeo ya hukumu hiyo.

Kamati ya Sheria ilikutana mara mbili kusikiliza shauri la Kagera na juzi lilitoa maamuzi ya kuirejeshea Kagera pointi zake tatu dhidi ya Simba, hasa baada ya kubaini madudu yaliyofanyika katika hukumu iliyowapa Simba ushindi.

Uchunguzi tulioufanya tangu mchakato huo uanze umebaini yafuatayo;

MJUMBE MWALIKWA

Katika hali ya kushangaza Kamati ya Saa 72 ilifanya kosa kubwa la kufanya vikao vyake viwili, wakiwa na mjumbe mwalikwa kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambaye ni mmoja ya mabosi wa Simba.

Kamati ilimpa nafasi mjumbe huyu (jina tunalo) aingie katika kikao hicho na hata kushiriki kuchangia kwa kile kinachoelezwa na wajumbe halali wa kikao.

UTATA TAARIFA ZA WAAMUZI

Kikao cha Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji uchunguzi umeonyesha kwamba hakikufika kujadili masuala ya kadi endapo Fakhi ana kadi tatu au vinginevyo lakini msukumo mkubwa wa hili umetokana na mkanganyiko wa taarifa za waamuzi.

Waamuzi wetu wamekuwa na mwendelezo wa utata wa maamuzi yao na hili pia limechomoza katika sakata hili, kanuni zinasema wazi kwamba mwamuzi wa kati ripoti yake ndiyo kitu kinachotakiwa kuheshimiwa lakini hapa kwetu tukisimamia katika hoja hii soka litapotea kama yalivyotokea kwa mwamuzi wa mchezo wa African Lyon dhidi ya Kagera Sugar.

Kamati ilichukua hatua za kuwahoji waamuzi wote wa mchezo, lakini katika mazingira ya hatari matokeo ya mchezo huo yaliyopo katika kitengo cha takwimu za bodi ya ligi hayaendani na yale ya mwamuzi wa kati wa mchezo.

Unaweza kujiuliza uko wapi tena usafi wa kufuata ripoti ya mwamuzi wa kati?

Matokeo yake baada ya kamati kuwahoji waamuzi wengine, wakabaini matokeo ya mchezo huo yaliyopo bodi ya ligi yalikuwa yakiendana na yaliyoletwa na mwamuzi mmoja tu.

“Ni hivi, ripoti ya Kamisaa ilionyesha mechi ya Lyon na Kagera matokeo yalikuwa 2-1 wakati ya mwamuzi ilikuwa 2-0, ila Bodi ya Ligi ilinukuu matokeo ya kamisaa,” mjumbe mmoja wa kamati ya Sheria alisema.

KIKAO CHA WAAMUZI CHAKATALIWA

Kuonyesha kwamba kuna kitu sehemu, kila mchezo unapomalizika, kikao cha waamuzi wote waliosimamia mchezo hukutana na kufanya kikao kifupi cha marejeo ya mechi ilivyochezwa.

Hata hivyo, kamati ya sheria imegundua kuwa kikao cha mchezo huu wa Lyon na Kagera hakikufanyika, hivyo mambo kufanyika kienyeji kitu ambacho ni hatari.

MCHEZO WAKWEPESHWA ‘LIVE’

Mchezo wa Lyon na Kagera ulichezwa katika mazingira tata na haukutakiwa kuonyeshwa mubashara kutokana na mazingira yaliyokuwapo na inaelezwa hii ndiyo chanzo na kwamba kilirahisisha mipango.

Azam Media haikupewa notisi ya kuwepo kwa mechi hiyo na hata kuweza kurekodiwa endapo suala la kuonyesha mubashara limeshindikana na hata kurekodiwe kwa lengo la kutunza kumbukumbu jambo ambalo halikufanyika.

Jambo hilo kwa sasa limeleta ukakasi mkubwa katika kutumia mkanda huo ambao ungesaidia kamati hizi kuweza kuondoa utata wa uwepo wa kadi.

OFISA WA BODI NA RIPOTI ZA WAAMUZI

Uchafu uliobainika ni kwamba ripoti ya mwamuzi wa mchezo kutumwa katika barua pepe (email) binafsi ya mmoja wa Maofisa wa Bodi ya Ligi kinyume na utaratibu wa kiofisi.

Kilichopaswa kufanyika ni kwamba barua pepe hizo za ripoti za mchezo wowote kutoka kwa waamuzi zilipaswa kutumwa katika akaunti ya Bodi ya Ligi moja kwa moja na siyo kwa ofisa yeyote jambo ambalo hapa kwetu limefanyika na lipo kama lilivyojiri nyakati hizi hadi Fakih kuja kutufichulia haya.

KIKAO CHAVUJISHWA SIMBA

Habari za ndani zinadai kwamba wakati kikao cha kwanza cha Kamati ya Sheria kikifanyika bila kujitambua, kumbe kikao hicho kilikuwa mubashara kwa njia ya simu baada ya mjumbe mmoja wa kamati ambaye ana uhusiano na moja ya klabu za Kagera na Simba kuvujisha.

Inadaiwa aliingia na simu na kuiwasha ili kunasa kila kilichokuwa kikijadiliwa au kuleta mvutano, huku mabosi wa moja ya klabu hizo wakisikiliza kinachoendelea bila mabosi wa Kamati ya Sheria kujua lolote.

Hata hatua ya kutaka kukimbilia kwenye vyombo vya dola kwa uchunguzi wa kina kwa yale waliyokuwa wamebaini katika kikao hicho cha kwanza, zilifika mapema kwa walengwa na kuanza kutengeneza mipango madhubuti kuyeyusha.

Athari ya hili ni kwamba baada ya kikao hicho kumalizika na maazimio kadhaa kuchukuliwa kwa kutaka kupata ukweli zaidi katika kikao cha pili mambo ya msingi yalivuja na ushahidi kupotea kwa wahusika kuwahi kurekebisha mambo.

BOSI WAAMUZI CHUPUCHUPU

Baada ya kamati hiyo kubaini mambo kadhaa ya kimapungufu katika waamuzi wa soka kamati ilikaribia kutaka kupitisha adhabu kwa kiongozi wa waamuzi aliyetuhumiwa kuongoza uharamia wa kupanga waamuzi kwa masilahi binafsi.

Hata hivyo, bosi huyo alisalimika baada ya hoja hiyo kupingwa vikali na baadhi ya wajumbe waliomtetea, ingawa ni kweli amebainika ni jipu kwa soka la Tanzania.

TFF, TPBL ZIMULIKWE

Ili kuweka mambo sawa kunahitaji jitihada za makusudi kuondoa baadhi ya watendaji wenye mashaka ndani ya TFF na Bodi ya Ligi (TPBL) wanaodaiwa kutumia nafasi zao kufanya kazi kwa masilahi ya ushabiki kwa kuzibeba timu zao.

Kikao hicho cha Sinamtwa na wenzake kimebaini utata mkubwa ikiwamo ilikuwaje rufaa ya Simba ilipitishwa na kusikilizwa Kamati ya Saa 72 ikiwa na mapungufu ya uwasilishwaji wake na mbaya zaidi viongozi wa TFF na TPBL walishiriki kulisimamia, ilihali ni hao hao walioitupilia mbali rufaa ya Polisi Dar es Salaam.

Polisi walicheleweshwa rufaa yao kwa saa chache walipokuwa wakiipinga Simba kwa kumtumia beki Novaty Lufunga aliyekuwa na kadi nyekundu aliyopewa msimu uliopita katika michuano ya Kombe la FA.

Wakati Simba inaumia baada ya kupokonywa pointi, sasa ni wazi kinachotakiwa kutumika kwa uamuzi wa Bodi ya Ligi kuangalia uhalali wa Kagera kupokwa pointi kwa kigezo cha kikanuni kwamba mchezaji mwenye kadi hatakiwi kusubiri kukatiwa rufaa.

Hilo lingeanza kufanyika wakati wa sakata la Lufunga, lakini kwa makusudi zilipindishwa kanuni ili kuibeba Simba, kitu kinachoipunguzia Shirikisho la Soka nchini (TFF) heshima mbele ya mashabiki wa soka nchini. Kama kanuni zingezingatiwa utata wote usingekuwepo katika sakata hili la pointi za Kagera.