Simbu ajitabilia medali

Muktasari:

Simbu aliyesema hayo baada ya kuwasili Arusha akitokea England alipokwenda kushiriki mashindano ya London Marathon yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mwanariadha Alphonce Simbu amesema kushika nafasi ya tano katika mashindano ya London Marathon ni fahali kubwa kwake na taifa kutokana na ukubwa wa mbio hizo duniani.

Simbu aliyesema hayo baada ya kuwasili Arusha akitokea England alipokwenda kushiriki mashindano ya London Marathon yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.

"Tanzania tunakazi kubwa mbele yetu katika kufanikiwa katika riadha, mataifa mengine yamejipanga vyema kwa serikali zao zinaunga mkono katika kuinua vipaji vya mchezo huu, lakini hapa kwetu mwamko upo chini naomba serikali itazame huku pia."

Simbu ameeleza changamoto inayomkabili ni kuwa mwenyewe kwenye kambi huku wengi wakiwa ni wanariadha wa mbio fupi hivyo kumfanya kutokuwa na ushindani anapofanya mazoezi.

"Mnapokuwa na kambi inasaidia vitu vingi kama chakula, muda na uangalizi wa makocha maalumu siyo kila siku unakua na walimu tofauti na unabadilishiwa mazoezi kwa kuwa kila mwalimu na ujuzi wake."

"Siku zote anayekushinda ni yule aliyekuzidi uwezo hivyo walishinda Londoni Marathoni ni kweli walinizidi, lakini mwezi wa nane kwenye mashindano ya dunia mimi na wenzangu tuliopata nafasi ya kuiwalikisha nchi mbio hizo nahaidi kwenda kufanya vizuri na hata kurudi na medali" alisema Simbu.

Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Iddy Kimanta akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alisemamwanariadha huyo ni balozi wa kutegemewa kwa sasa kutokana na kuipeperusha vyema bendera ya nchi kwenye mashindano mbalimbali na makubwa.

"Kiwango chake kimeimalika kila mara tofauti na muda aliotumia Michezo ya Olimpiki mwaka jana, London Marathon katumia Saa 2:09:10 huku bingwa Daniel Wanjiru raia wa Kenya akitumia Saa 2:05:48," alisema Kimanta.