Simba yapiga mtu 2G Dar

Muktasari:

  • Bao la dakika ya nne kupitia winga Pastory Athanas ambalo ni la kwanza kwake tangu ajiunge Simba na la pili la dakika ya 83 likifungwa kwa kichwa na beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ yalitosha kuipa ushindi muhimu vijana wa Joseph Omog waliodhibitiwa vilivyo na vijana wa Polisi.

POLISI Dar jana Jumapili waliingia kichwakichwa Msimbazi na kujikuta wakigongwa mabao 2-0 na Simba katika mechi ya raundi ya tano ya Kombe la FA.

Simba ilipata ushindi huo katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na kuifuata Yanga iliyosonga mbele tangu juzi kwa kuichapa Ashanti United kwa mabao 4-1.

Bao la dakika ya nne kupitia winga Pastory Athanas ambalo ni la kwanza kwake tangu ajiunge Simba na la pili la dakika ya 83 likifungwa kwa kichwa na beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ yalitosha kuipa ushindi muhimu vijana wa Joseph Omog waliodhibitiwa vilivyo na vijana wa Polisi.

Polisi iliangushwa tu na kukosa uzoefu, lakini vijana wao walijitahidi kuwabana nyota wa Simba kwa vipindi vyote vya mchezo huo uliokuwa mkali. Mabadiliko yaliyofanywa kipindi cha pili na Kocha Omog akiwatoa Ibrahim Ajib, Mwinyi Kazimoto na Athanas kuwapisha, Said Ndemla, Jamal Mnyate na Laudit Mavugo yalileta uhai kwa Simba mpaka walipopata bao lao la pili.

Katika mechi nyingine za Kombe la FA, Prisons ikiwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya iliitambia Mbeya Warriors kwa mabao 2-1. Mabao yaliyofungwa dakika ya 3 na Emmanuel Mnyali na Mohammed Samatta dakika ya 54, huku la Mbeya Kwanza likifungwa kwa penalti na Eliuter Mpepo dakika ya 30.

Ruvu Shooting iliaibishwa na Kiluvya Utd kwa kufungwa 2-1 kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani, wakati kutoka Mwanza, Toto Africans ilishinda kwa penalti 5-4 baada ya kumaliza dakika 90 na Mwadui kwa sare ya mabao 2-2.

Michuano hiyo itaendelea tena leo Jumatatu kwa Azam kuikaribisha Cosmo, Polisi Mara itaumana na Stand United na Ndanda itavaana na Mlale JKT.

Nyongeza imeandikwa na Saddam Sadick-Mwanza na Godfrey Kahango-Mbeya.