Simba yapania kuvunja rekodi ya Mgosi

VINARA wa Ligi Kuu Bara, Simba msimu wa 2009/10 iliweka rekodi ya kushinda mechi 14 mfululizo na kunyakua ubingwa bila kupoteza hata mechi moja, huku aliyekuwa nyota wao, Mussa Hassan Mgosi akiibuka Mfungaji Bora akiwa na mabao 16.

Lakini, kwa sasa akiwa kama Meneja wa Simba, Mgosi ameapa kuona rekodi hiyo ya msimu wa 2009-2010 ikivunjwa na kikosi anachokiongoza sasa kinachonolewa na Kocha Joseph Omog akisaidiana na Jackson Mayanja.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mgosi alisema ingawa msimu huu imeshindwa kushinda mfululizo, lakini watapigana ili kumaliza msimu bila kupoteza mechi kama ilivyokuwa msimu huo na kutoa Mfungaji Bora.

Mgosi alisema mpaka sasa Simba ikiwa imecheza mechi 11 haijapoteza hata mchezo mmoja, huku Shiza Kichuya akiongoza orodha ya wafungaji kitu ambacho anaamini kitaendelea hadi mwisho wa msimu wa kuvunja rekodi.

“Kipindi hicho Simba, ilicheza mechi 14 bila kupoteza, kabla ya kulazimishwa sare katika mechi zote na kubeba taji huku nikiibuka Mfungaji Bora, hata msimu huu inawezekana,” alisema.

Aliongeza kuwa kazi yake kwa sasa ni kuwahamasisha wachezaji kujitoa kikamilifu kwa manufaa ya timu ili kurejesha heshima ya Wekundu wa Msimbazi.

SIMBA KUPANDA NDEGE

Mgosi pia amesikia kejeli zinazotolewa na watani zao wa Yanga juu ya timu yao kupanda ndege kwenda Kanda ya Ziwa na kusema mbona hiyo sio ishu, kwa sababu wakiangalia vizuri rekodi za nyuma Simba wamekwea sana pipa kuliko timu yoyote nchini.

“Wasipende kuropoka tu,  tangu Simba na Yanga, zianzishwe waangalierekodi vizuri nani anaongoza kwa kupanda ndege, pia ni maamuzi ya timu kupanda ndege na sio ishu kivile. Sema wanataka kuwazingua wachezaji wetu kiakili, ila wamenoa kwa sababu msimu huu tupo makini,” alisema.