Simba yanyakua mido mpya, yahama uwanja wa Zanzibar

Muktasari:

  • Huo ni usajili wa pili wa Simba ambayo hivi karibuni ilimsajili kiungo mshambuliaji wa Coastal Union, Ibrahim Twaha 'Messi'. Dilunga yumo kwenye kikosi cha Young Taifa Stars chini ya kocha Kim Poulsen.

SIMBA hawataki mchezo, wamemsajili kiungo mwingine mshambuliaji wa Ruvu Shooting, Hassan Dilunga tayari kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Mchezaji huyo anasifika kwa utulivu na ufundi wa mpira uwanjani pamoja na uwezo wa kutoa pasi za mwisho zenye macho.

Huo ni usajili wa pili wa Simba ambayo hivi karibuni ilimsajili kiungo mshambuliaji wa Coastal Union, Ibrahim Twaha 'Messi'. Dilunga yumo kwenye kikosi cha Young Taifa Stars chini ya kocha Kim Poulsen.

Mwanaspoti linajua kwamba Dilunga pamoja na uongozi wa Ruvu Shooting wamemalizana na atatua Msimbazi msimu ujao. Mchezaji huyo alipoulizwa na Mwanaspoti alisema: "Ni kweli Simba wamenifuata kuzungumza nami juu ya usajili lakini bado hatujafikia makubaliano, bado nina mkataba wa mwaka mmoja na Ruvu Shooting ni jukumu la Simba kumalizana na uongozi wangu,"alisema Dilunga ambaye Mwanaspoti linajua kuwa Simba imeshamaliza na mabosi wake na kuafikiana.

Dilunga alifafanua kuwa, suala la yeye kusajiliwa Simba amelisikia kwa watu mbalimbali akiwemo katibu wake wa Ruvu, Issa Mikweli. Ameongeza na kusema kama uongozi huo utamalizana na timu yake na ukampa maslahi ya kuridhisha atakuwa tayari kujiunga nao.

Mchezaji huyo hakuwemo katika safari na klabu yake ya Ruvu Shooting ilipoenda kucheza na Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba Jumamosi iliyopita matokeo yakawa sare ya 1-1 na akaeleza kuwa alikuwa na mambo binafsi ndiyo maana hakujiunga na timu hiyo.

Mwenyekiti wa Usajili wa Simba, Zakaria Hanspope alipoulizwa hakutaka kufafanua kwa madai kuwa bado muda na kwamba sasa wanaangalia kwanza mechi na Yanga Jumamosi.

Wakati huo huo MFARANSA wa Simba, Patrick Liewig ameendelea na dozi ya mazoezi mara mbili kwa siku kuhakikisha kikosi chake kinakuwa fiti na kinajenga kujiamini zaidi kwa mechi dhidi ya Yanga Jumamosi ijayo.

Liewig amewahamisha nyota wake kutoka Uwanja wa Chuo cha Chukwani waliokuwa wanautumia na kuwapeleka Mao Tse Tung ambao ni bora na umetulia zaidi na ni ngumu kwa Yanga kupenyeza mashushu wao kirahisi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Liewig alisema: "Tunaendelea na mazoezi kama kawaida ambapo kwa siku ya leo (jana Jumatatu),  kesho (leo Jumanne) na Jumatano tutafanya asubuhi na jioni."

"Kambi ipo tulivu na mazingira ni mazuri na lengo kuu ni kuwafanya wachezaji wawe katika hali ya mchezo tayari kwa mechi hiyo ya Jumamosi, Tumehama Uwanja wa Chukwani na kuwahamisha pengine,"alisema Liewig.

Uwanja wa Chukwani unadaiwa haukuwa katika hali nzuri kwa kufanyia mazoezi kutokana na kuwa na nyasi ndefu zinazotakiwa zikatwe na kuandaliwa vizuri.

Mwenyeji wa Simba Zanzibar ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Simba, Abdul Mshangama alisema: "Hali ya kambi ni safi kabisa, timu inapata huduma zote kuhakikisha tunatimiza malengo yetu. Tayari tumepata Uwanja wa Mao kwa ajili ya mazoezi kwa sababu ule wa Chukwani mwalimu hakuupenda."

Mechi ya Jumamosi itakuwa ni ya kukamilisha ratiba kwani tayari Yanga ni mabingwa wa Ligi Kuu Bara.

Katika hatua nyingine, benchi la ufundi la Yanga linaloongozwa na kocha Mholanzi, Ernie Brandts amesifu mazingira ya kambi yao Kisiwani Pemba pamoja na Uwanja wao wa mazoezi wa Gombani kuwa unawapa hari ya ushindi nyota wake.

Yanga inajiandaa na mechi yao ya Watani wa jadi Simba mchezo utakaochezwa Jumamosi ijayo Mei 18 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizunzungumza na Mwanaspoti, Brandts alisema: "Mazingira ya kambi ni mazuri, Uwanja mzuri na hali ya hewa pia ni nzuri."

"Tunaendelea na maandaalizi yetu katika mahali tulivu na kubwa ni kuwajenga wachezaji kisaikolojia wawe katika hali ya mchezo,"alisema Brandts.

Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh naye amesifu kambi hiyo kuwa ni nzuri hasa uwanja huo wa mazoezi wa Gombani.