Simba yamshushia Mkude Mido Mghana

Muktasari:

Habari za ndani zinadai kwamba mchezaji huyo anaandaliwa kuchukua nafasi ya Mkude ambae ni nahodha wa Simba anayemaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huku akihusishwa na timu moja ya Afrika Kusini.

SIMBA jana ilitarajia kushusha kiungo mkabaji kutoka Ghana, James Agyekhum Kotei kwa ajili ya mazungumzo ya mwisho na kumpa mkataba. Kiungo huyo maarufu kama Lampard nchini Ghana lazima ameletwa mahususi baada ya kiungo Jonas Mkude kuonekana kuzozana na baadhi ya viongozi kuhusiana na hatma ya mkataba wake mpya.

Habari za ndani zinadai kwamba mchezaji huyo anaandaliwa kuchukua nafasi ya Mkude ambae ni nahodha wa Simba anayemaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huku akihusishwa na timu moja ya Afrika Kusini.

Tayari Simba hadi sasa ina wachezaji saba wa kigeni huku kipa kutoka Ghana, Daniel Agyei aliyetokea timu ya Medeama ambaye jana Jumatatu alisaini mkataba na Wekundu hao wa Msimbazi akisubiri nafasi ya mmoja ikatwe ambapo Mussa Ndusha na Juuko Murshid mmoja wao ana nafasi kubwa ya kupewa mkono wa kwaheri.

Mwingine anayepumulia mashine pia ni Janvier Bokungu huku Method Mwanjali, Laudit Mavugo na Fredrick Blagnon wakiwa na uhakika na maisha ndani ya Simba. Kwa mara ya mwisho, Kotei aliichezea timu ya Al-Oruba ya Oman lakini alishindwa kumalizia mkataba wake baada ya timu hiyo kushindwa kumlipa ingawa kwao Ghana alizichezea timu kama Liberty Professionals FC pamoja na BA Stars.

Habari kutoka ndani ya Simba, zilisema kuwa Kotei ambaye atakuwa Mghana wa pili ndani ya Simba atampa changamoto Jonas Mkude ambaye anawaringia Simba kusaini mkataba mpya baada ya huu wa awali kubaki miezi sita. Mkude na Ibrahim Ajibu wanatajwa kutaka kuondoka Simba na wanasubiri mikataba yao imalizike ili waondoke bila gharama.

“Kotei anawasili leo (jana), tutamfanyia vipimo kama ilivyokuwa kwa Agyei ndipo tutaingia naye mkataba, hawa wachezaji wetu wazawa muda mwingine wanakuwa wasumbufu, Mkude na Ajibu wamekuwa wakibembelezwa kusaini mikataba mipya lakini hawaonyeshi nia hivyo ni vyema tukawa na wengine watakaowapa changamoto,” alisema kiongozi huyo.

Mwishoni mwa wiki, uongozi wa Simba uliwaeleza viongozi wa matawi yao juu ya usumbufu wanaoupata kwa wachezaji hao wanaoshindwa kumalizana na klabu hiyo ambapo wanachama hao walitoa angalizo kwamba wakigoma kabisa ni vyema waachane nao ili wamalize mikataba yao na waondoke.