Simba yaitia aibu Yanga Dar

Muktasari:

Mastaa wengi wa Simba wameonekana kutamba na Stars na kupunguza kelele za Yanga waliokuwa wakitamba kwamba wao ni wa kimataifa.

KITENDO cha Yanga kusajili wachezaji wa gharama kubwa kutoka nje ya nchi kimewaponza kwani katika kikosi cha Taifa Stars sasa kuna mchezaji mmoja tu anayeanza kati ya wachezaji wanne walioitwa.

Licha ya kwamba ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara na timu iliyoshiriki michuano ya kimataifa kwa miaka minne mfululizo sasa, imejikuta ikizidiwa ujanja na Simba kwenye timu ya Taifa.

Mastaa wengi wa Simba wameonekana kutamba na Stars na kupunguza kelele za Yanga waliokuwa wakitamba kwamba wao ni wa kimataifa.

Katika miaka ya karibuni Yanga imekuwa na jeuri ya fedha za Mwenyekiti wao Yusuf Manji na imekuwa ikifanya usajili wa kufuru kwa kuwaleta mastaa wakubwa kutoka nchi za Zimbabwe, Zambia, Rwanda na Burundi kitendo ambacho kimewaponza sasa.

Katika mchezo wa juzi Jumamosi dhidi ya Botswana, Saimon Msuva ndiye mchezaji pekee wa Yanga aliyeanza kwenye kikosi cha Stars huku pia kukiwa hakuna mchezaji yeyote mwingine wa timu hiyo aliyeingia hata kama chaguo la pili.

Katika kikosi cha kwanza cha Stars, Azam ndiyo iliyokuwa na wachezaji wengi zaidi na nyota watano wa timu hiyo walianza sambamba na wanne wa Simba, mmoja wa Yanga pamoja na staa wa timu, Mbwana Samatta anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji. Licha ya kwamba Yanga ilikuwa na Msuva pekee uwanjani, nyota wengine walioitwa ambao hawakucheza ni kipa Deo Munishi ‘Dida’, mabeki Andrew Vincent ‘Dante’, na Hassan Kessy.

Wachezaji wa Simba walioanza katika mchezo huo ni Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Shiza Kichuya na Ibrahim Ajibu. Nyota wengine wa Simba, Mzamiru Yassin, Jonas Mkude na Said Ndemla waliingia kipindi cha pili hivyo kufanya wachezaji waliocheza mchezo huo kufikia saba.

Mabadiliko hayo ya Simba kuingiza wachezaji wengi katika timu ya Taifa yameshtua kutokana na ukweli kwamba mwaka mmoja uliopita timu hiyo ilikuwa na mchezaji mmoja tu anayeanza katika kikosi hicho huku Yanga ikiwa imetawala kila idara. Mchezaji wa Simba aliyekuwa anapata nafasi ni Mkude pekee.

Nyota wa zamani wa Yanga, Aaron Nyanda alisema; “Hatuwezi kusema kwamba Yanga ina kikosi kibaya sana kwa sasa, hapana. Wachezaji wa kigeni wa Yanga wanafanya vizuri katika nafasi ambazo wachezaji wazawa wa Simba na Azam wanafanya vizuri pia, katika timu ya taifa lazima wakose wawakilishi wengi.

“Mfano viungo Thaban Kamusoko na Haruna Niyonzima ndiyo viungo bora kwenye Ligi Kuu lakini sio wazawa, hii inatoa nafasi kwa viungo wa Simba na Azam kupata nafasi,” alisema Nyanda ambaye alicheza Toto Africans na Yanga tu.

“Yanga ina wachezaji kutoka Zanzibar wanaofanya vizuri pia lakini hawakupewa nafasi kutokana na eneo lao la nchi kupewa uwakilishi katika mashindano ya CAF. Nadhani kocha aliamua kutengeneza kikosi chenye sura ya Bara,” alieleza.

Kocha msomi zaidi nchini, Profesa Mshindo Msola alisema kinachoiponza Yanga ni baadhi ya nyota wake kushindwa kupambania nafasi zao mbele ya wachezaji wa kigeni tofauti na nyota wa Simba na Azam.

Msola alisema Simba pia imekuwa makini katika usajili wake kwa kutafuta wachezaji wenye vijapi vikubwa na kuwalea kitendo ambacho kimewapiga bao watani zao Yanga ambao wamejikita zaidi katika kutegemea wageni.

“Makocha wengi wa Yanga wamekuwa sio watu wa kuwaamini wachezaji na kuwajenga. Wengi wanataka wachezaji ambao wako tayari na wanaweza kufiti moja kwa moja kwenye timu. Wachezaji wengi wanakwenda Yanga wakiwa wazuri lakini hawaaminiwi na mwishowe wanakosa nafasi timu ya taifa.

“Pia nailaumu TFF kwa kuruhusu wachezaji saba wa kigeni kwani hili limewafanya Yanga kulala. Timu hiyo inatazama zaidi nje na imeshindwa kuwasaidia wachezaji wetu. Viongozi wa Yanga wabadilike,” alisema.