Simba wamalizana na wachezaji

Muktasari:

Simba inaonekana kujipanga mapema ili kuweza kutawala soka la Tanzania kwani katika kikosi chake cha kwanza ni wachezaji wawili tu ambao wanamaliza mikataba yao na wamelazimisha kuondoka tofauti na watani zao hao ambapo nusu ya kikosi chao inamaliza mikataba.

MABOSI wa Simba wametazama idadi kubwa ya nyota wanaomaliza mikataba katika kikosi cha watani zao Yanga na kubaini kuwa wana nafasi ya kuipiga bao timu hiyo mapema na kujitengeneza ufalme.

Simba inaonekana kujipanga mapema ili kuweza kutawala soka la Tanzania kwani katika kikosi chake cha kwanza ni wachezaji wawili tu ambao wanamaliza mikataba yao na wamelazimisha kuondoka tofauti na watani zao hao ambapo nusu ya kikosi chao inamaliza mikataba.

Nyota wa Simba wanaomaliza mikataba na wameshinikiza kuondoka mpaka sasa ni Ibrahim Ajibu na Jonas Mkude ambaye hata hivyo tayari mbadala wake ameshapatikana. Nyota anayeandaliwa kurithi mikoba ya Mkude ni Mghana James Kotei ambaye tayari ameanza kupata nafasi katika kikosi cha kwanza.

Nyota wengine waliokuwa wanamaliza mikataba yao na tayari wameongezwa ni Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ huku Abdi Banda akiwa tayari katika mazungumzo ya mwisho ya kuongeza mkataba.

Nyota wa kikosi cha kwanza wa Yanga wanaomaliza mikataba yao ni mabeki Mwinyi Haji na Vincent Bossou, viungo Haruna Niyonzima na Thaban Kamusoko pamoja na mshambuliaji Donald Ngoma.

Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema wamehakikisha kwamba wanaendelea kubaki na wachezaji wote muhimu hasa waliopo katika kikosi cha kwanza kutokana na ukweli kwamba wengi wao bado ni vijana wadogo. Kaburu alisema hata wachezaji ambao mikataba yao inamalizika bado wapo katika mazungumzo nao kuona kama wanaweza kuwabakisha ikiwa ni jitihada za kujenga timu imara zaidi kwaajili ya msimu ujao wa mashindano.

“Tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwabakisha wachezaji muhimu, bado tupo kwenye utaratibu wa kuzungumza na wengine ambao walionyesha nia ya kuondoka. Nia yetu ni kuhakikisha wachezaji wote mahiri wanabaki,” alisema.

 

MO ATIA NDIMU

Katika hatua nyingine, Kaburu alisema mambo matatu ndiyo yamewabeba na kuweza kuongoza Ligi Kuu mpaka sasa ambapo mojawapo ni kujitolea kwa bilionea Mohammed Dewji kuwalipa mishahara wachezaji tangu mwezi Septemba mwaka jana.

“Wanachama wamekuwa pamoja kwa wakati wote. Wamekuwa wakitoa michango kuhakikisha wachezaji wanapata posho nzuri na wanasafiri vizuri. Viongozi pia tumekuwa makini katika kuwaunganisha wanachama hawa na kutumia fedha zinazopatikana vizuri.

“Tumekuwa na mchango mkubwa pia kutoka kwa Mohammed Dewji, amekuwa akilipa mishahara tangu Septemba mwaka jana na ndiyo sababu unaona kuwa hatuna matatizo yoyote ya mishahara katika timu yetu,” alisema Kaburu.