Simba na Mbao kazi ipo Dodoma

Muktasari:

Simba na Mbao zitapambana katika fainali ya FA itakayofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma. 

KOCHA msaidizi wa Njombe Mji, Mrage Kabange ameionya Simba kuwa inatakiwa kuwa makini sana katika fainali yao ya FA dhidi ya Mbao kwani inaweza kuwaachia machungu wasiyoyategemea.

Simba na Mbao zitapambana katika fainali ya FA itakayofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.

Mrage ambaye ni mwanachama hai wa Simba, alisema jambo la kwanza litakalowapa shida Simba ni uwanja kwani wekundu hao wa Msimbazi wameonekana kupata shida katika viwanja vibovu.

“Kwanza Simba imeonekana inapata shida viwanja vya mikoani ambavyo haviko katika hali nzuri kama Taifa sasa jambo hilo linaweza kuwagharimu kama hawajalifanyia mazoezi.

“Pia mechi ya ligi Simba iliifunga Mbao akitoka nyuma kwa mabao mawili na kushinda tatu, sasa hiyo inaonyesha jinsi gani mechi hiyo ya fainali itakavyokuwa siyo ya kitoto kwani Mbao hivi sasa wamejiamini na watajizatiti, hawatakuwa na uoga tena,” alisema Mrage.

Aliongeza, “Halafu Simba itaikabili Mbao ikiwa kwenye presha kubwa ya ushindi kwani tayari bingwa wa ligi ameshajulikana na nafasi iliyobaki kushiriki kimataifa ni kushinda fainali ya FA, sasa kama wachezaji wa Simba hawataandaliwa kisaikolojia wanaweza kupoteza mchezo huo.

MSIKIE MAGANGA

Straika wa Mbao FC, Boniface Maganga amefunguka na kudai watayafanyia kazi makosa yaliyowagharimu dhidi ya Simba katika mechi mbili zilizopita ili kuondoka na mwali wa Kombe la FA.

Mshindi wa mchezo huo mbali na kupewa kombe na Sh 50 milioni, pia atawakilisha nchi katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani. Mbao imekuwa tishio kwa siku za karibuni hasa baada ya kuifunga Yanga mara mbili