Simba andaeni suti za ubingwa kabisa

Muktasari:

Mchezaji huyo amesisitiza kwamba anaelewa kero wanazokumbana nazo mashabiki wa Simba mitaani kwa kejeli za Yanga, hivyo anataka kufanya mambo ili Msimbazi nao wapate cha kujivunia.

SHIZA Kichuya amewaambia mashabiki wa Simba kwamba anajua wanamdai baada ya kushindwa kuwapa ubingwa wa Ligi, lakini kesho Jumamosi kama kocha, Joseph Omog,  atampanga basi atawalipa.

Kichuya amemaliza msimu akiwa na mabao 12, ameweka wazi kitakachofuta machungu ya kuukosa ubingwa ni kuifunga Mbao FC hiyo kesho katika fainali ya Kombe la FA mjini Dodoma. Mchezaji huyo amesisitiza kwamba anaelewa kero wanazokumbana nazo mashabiki wa Simba mitaani kwa kejeli za Yanga, hivyo anataka kufanya mambo ili Msimbazi nao wapate cha kujivunia.

Alienda mbali zaidi na kuonyesha kukerwa na nyodo za mastaa wa Yanga ambao walikatiza Msimbazi na kombe na kuanza kubugudhi mashabiki na wanachama wa Simba.

“Ninafurahia kufanya kitu kilichoonekana, lakini kumbuka kuna maendeleo ya klabu nikimanisha Kombe la FA, linatakiwa kutua Msimbazi ili mashabiki walipokee na kupiga nalo picha kama ilivyo kwa watani wetu Yanga, ndiyo maana nimesema nafasi pekee ya kufuta machungu, nikupambana hadi nukta ya mwisho,” alisema.

“Nikizungumzia mbinu mpya kwenye mchezo wa Mbao ni kutumia staili ambayo hatujawahi kuitumia ligi kuu, naamini hiyo ndiyo njia pekee ambayo tutafanya mashabiki wetu wawe huru mitaani kwani ni kitu ambacho kinatolewa macho na wadau wengi nchini.

“Ni miaka mitano sasa hakuna taji lililotua Msimbazi na hii ndiyo nafasi pekee kwa wachezaji kufufua matumaini kwa mashabiki ambao wanatusubiria kwa hamu na wengine wapo na presha tupu kikubwa Mungu atusaidie tu.”

Alitaja ugumu mwingine kuwa ni  kitendo cha kumalizika kwa ligi na kutokuwepo michuano inayoendelea zaidi kujua nani atakuwa bingwa wa FA,kitu alichodai kinachangia presha kwa mashabiki wa Simba.

WACHEZAJI MAZOEZINI

Simba iliwasili Dodoma jana Alhamisi, lakini kocha wake, Mcameroon Joseph Omog, amefurahishwa na morali waliyoionyesha wachezaji wake ambao licha ya kufanya mazoezi kwenye mvua wao ndiyo kwanza walichekelea.

Kikosi hicho, kilianza kambi tangu wikiendi iliyopita na kufanya mazoezi yao Uwanja wa Jamhuri Morogoro kujiandaa na mchezo huo.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu, Omog alisema: “Tumefanya maandalizi mazuri na wachezaji wana morali ya juu, kwani licha ya kufanya katika mazingira magumu ya mvua, hakukuwa na tatizo lililojitokeza, zaidi walijitolea  kama hakukuwa na hali hiyo.

“Tunaendelea na maandalizi yetu kama kawaida na sasa tuko vizuri hata ikitokea mchezo huo ukachezwa katika mazingira ya mvua hatuna wasiwasi, mazingira yake yatatusaidia kwa namna moja ama nyingine katika mchezo wetu.”

Hata hivyo, kutokana na mazingira ya hali ya hewa ya sasa, mvua kunyesha mara kwa mara kama  itakuwa hivyo, Simba wanaweza kupiga bao la maana kwa sababu watakuwa wameshayazoea mazingira ya namna hiyo kutokana na kuyafanyia  majaribio.

Kocha wa Mbao, Mrundi Etienne Ndayiragije, alisema: “Ninachopenda kusema ni kwamba mpira uchezwe uwanjani hapo ndiyo tutajua nani ni bora kuliko mwenzake, Simba siyo timu mbaya lakini hata sisi ni bora kuliko wao na ndiyo maana tumefika hatua hii na lengo letu ni moja tu kutwaa ubingwa huo, itawezekana tu endapo watachezesha kwa umakini.

“Kila mmoja anajiandaa na mechi itakuwa ngumu lakini naamini mambo yatatuendea vizuri kwa namna tulivyojiandaa.”