Madini kitu gani? Simba siyo ya mchezomchezo

MASHABIKI WA KLABU YA SIMBA

Muktasari:

  • Kocha wa Madini, Juma Abdallah alidai Simba walibahatisha. “Tumefungwa lakini furaha yangu ni kwamba, wachezaji wangu walionyesha kiwango cha juu mpaka mwisho. Simba ni timu kubwa kwa kiwango chetu cha daraja la pili, huenda tungefungwa hata mabao manane lakini tulipambana.”

WEKUNDU wa Msimbazi, Simba tayari imeshakata tiketi ya kucheza nusu fainali ya Kombe la FA na sasa wanawasubiri watani wao Yanga ambao watakapowasili tu kutoka Zambia watacheza na Tanzania Prisons robo fainali.

Licha ya Madini FC kuonyesha umahiri wa aina yake ndani ya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Simba walipata bao  dakika 54 kupitia kwa Mrundi, Laudit Mavugo kwa kichwa nje ya 18. Mpira uliozaa goli la ushindi ulikuwa ni shuti la moja kwa moja la mlinda mlango wa Simba, Daniel Agyei.

Kocha wa Madini, Juma Abdallah alidai Simba walibahatisha. “Tumefungwa lakini furaha yangu ni kwamba, wachezaji wangu walionyesha kiwango cha juu mpaka mwisho. Simba ni timu kubwa kwa kiwango chetu cha daraja la pili, huenda tungefungwa hata mabao manane lakini tulipambana.”

Kwa matokeo hayo, Simba pamoja na Mbao iliyoitoa Kagera Sugar itasubiri droo ya nusu fainali ichezeshwe mwishoni mwa mwezi huu baada ya mechi za Azam na Ndanda watakaocheza Chamazi huku Yanga ikiikabili Prisons, Taifa.

Mavugo kafunga bao hilo la sita mfululizo tangu alipoifunga Majimaji mechi ya ligi na baada ya hapo aliifunga Polisi Dar es Salaam, Prisons, Mbeya City, Yanga pamoja na Madini.

Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja raia wa Uganda alisema: “Madini ilitupa ushindani mkubwa. Tulipambana sana kupata matokeo.”

Mchezo huo Simba kupitia mabeki wake wa pembeni, Mkongo Besala Bokungu na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ walipandisha mashambulizi ya mara kwa mara na kupiga krosi lakini safu ya ulinzi ya Madini ilikuwa imara.  Dakika ya 58 Simba ilifanya mabadiliko kwa kumtoa, Mudhamiru Yassin na kumwingiza, Jonas Mkude na mabadiliko hayo yalikifanya kikosi hicho cha Mcameroon Joseph Omog kung’ara. Na kupitia kwa kiungo wao mwenye nguvu za miguu, Said Ndemla nusura wapate bao la pili dakika ya 62 lakini shuti lake lilitoka nje.