Simba: Yanga tunamnyoosha na ubingwa tunauchukua

Beki wa Azam, Gadiel Michael (kulia) akimdhibiti kiungo wa Simba, Jamal Mnyate wakati wa mchezo wa Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana. Azam ilishinda bao 1-0. Picha na Said Khamis.

Muktasari:

  • Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja ‘Mia mia’ alisema bado wana nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo

SIMBA imegoma kukubali kirahisi kuwa imepoteza hesabu za ubingwa wa Ligi Kuu Bara na sasa imefichua siri kuwa ni lazima washinde mechi zao 10 zilizosalia ikiwemo dhidi ya watani zao Yanga Februari 25 mwaka huu na kutwaa ubingwa.

Timu hiyo yenye mafanikio makubwa katika soka la Tanzania, ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Azam juzi Jumamosi lakini imegoma kuweka silaha chini na kudai kuwa bao vita ni mbichi kabisa na nafasi yao kutwaa ubingwa ni kubwa.

Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja ‘Mia mia’ alisema bado wana nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo ambapo sasa hesabu zao zinaonyesha ni lazima waifunge Yanga Februari 25 mwaka huu jambo ambalo linawezekana kabisa.

Mayanja ambaye amekuwa kocha msaidizi wa Simba kwa mwaka wa pili sasa, alisema licha ya kuwa na ratiba ya mechi nne ugenini bado wana imani kubwa kuwa wanaweza kushinda zote huku pia Yanga akiwa katika hatari ya kupoteza baadhi ya michezo.

“Tumepoteza pointi nyingi katika uwanja wa nyumbani, kwanza ni lazima tuhakikishe hatupotezi pointi yoyote ndani ya Dar es Salaam, bado ni jambo linalowezekana,” alisema Mayanja aliyewahi kuzinoa Kagera Sugar na Costal Union.

“Katika mechi 10 zilizosalia mambo mengi yanaweza kutokea lakini kwetu ni lazima tuhakikishe tunashinda mechi zote hasa zile sita ambazo tutacheza nyumbani.

“Uzuri ni kwamba katika ratiba hii tutakutana pia na Yanga ambaye tunakimbizana naye katika ubingwa, kwetu hii ni mechi ya lazima kushinda, kama tutapata matokeo katika mechi nyingine pamoja na hii ya Yanga ni wazi kwamba hesabu zetu zitakwenda vizuri,” alifafanua kocha huyo na kudai kuwa Aishi Manula ndiye aliyekuwa kikwazo kikubwa kwao kupata ushindi dhidi ya Azam.

Mogella agoma

Wakati benchi la ufundi la Simba likiwa na imani ya kutwaa ubingwa, nyota wa zamani wa timu hiyo, Zamoyoni Mogella ambaye pia mwanachama wa Simba, alisema sasa ndoto za ubingwa zimezimika rasmi klabuni hapo.

Mogella ambaye alicheza soka kwa kiwango cha juu, alisema lawama za kuporomoka kwa Simba zinakwenda kwa wachezaji na siyo benchi la ufundi kama watu wengine wanavyodai.

“Wachezaji wanacheza bila malengo, wanacheza kama watoto wadogo, yaani huoni kama kuna kitu wanataka katika mechi. Wanampa lawama za bure kocha, wanataka yeye aingie akafunge magoli?” Alihoji Mogella ambaye pia aliwahi kuichezea Yanga na Taifa Stars.

“Kwa upande wangu naona kutwaa ubingwa haiwezekani tena, tuliwaacha Yanga kwa pointi nane na sasa wanaweza kuanza kutuacha, tusitarajie makubwa tena,” alifafanua.