Simba, Yanga malizeni sakata la Hassan Kessy

Hassan Kessy

Muktasari:

Ndio maana mara kadhaa wadau wa michezo wamekuwa wakihimiza umuhimu wa kuwekeza kwenye michezo kuanzia ngazi za chini, ili kusaidia kujenga misingi imara itakayokuja kuleta tija mbeleni ya safari.

MAENDELEO ya soka na michezo mingine hujengwa katika misingi ya kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji kupitia vijana wadogo.

Ndio maana mara kadhaa wadau wa michezo wamekuwa wakihimiza umuhimu wa kuwekeza kwenye michezo kuanzia ngazi za chini, ili kusaidia kujenga misingi imara itakayokuja kuleta tija mbeleni ya safari.

Hata mataifa mengine yamekuwa yakifanikiwa na kuiacha mbali Tanzania kwa sababu ya kuelekeza nguvu kubwa kuwapa nafasi vijana kucheza na kuvidhihirisha vipaji vyao.

Kama vijana wanakwamishwa kuendeleza vipaji vyao ni vigumu soka ama michezo mingine kusonga mbele kwa sababu, kunakuwa hakuna warithi sahihi wa kushika nafasi za wakongwe au wachezaji wazoefu ambao umri huwa umewatupa mkono.

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na sintofahamu juu ya suala la beki wa pembeni wa Yanga aliyesajiliwa kutoka Simba Hassan Kessy.

Usajili wake ndani ya kikosi cha Jangwani umekuwa na utata mkubwa kutokana na mabosi wa zamani wa Simba kuendelea kung’ang’ania kuwa alikuwa ni halali yao na kusababisha mchezaji huyo mpaka leo kushindwa kucheza mechi za Ligi Kuu.

Yanga inalalamikiwa kuwa ilimsajili Kessy na kumtumia akiwa na mkataba na Simba, japo tayari kulikuwa na madai kwamba Simba ilishapanga kuachana naye kutokana na adhabu iliyompa, baada ya tukio lake la kupewa kadi kwenye mechi ya msimu uliopita.

Kessy alipewa kadi nyekundu katika mchezo wao na Toto Africans kwa kosa la kumchezea vibaya Edward Christopher na Simba ikatangaza kumfungia mechi tano kwa kosa hilo, huku mkataba wake ukiwa unaelekea ukingoni.

Kabla ya hapo beki huyo alishapata lawama kutokana na kosa alililofanya wakati Simba ikilala mabao 2-0 kwa Yanga na kuhisiwa kama aliyeifanyia hujuma, hivyo kwa adhabu aliyopewa ilionekana ni kama ule msemo wa akufukuzae hakuambii toka.

Yanga wakamdaka na kumfikisha hapo alipofikia akiwa ni mtazamaji wa wachezaji wenzake katika ligi inayoendelea. Mwanaspoti haitaki kumtetea Kessy wala Yanga ama kuilaumu Simba, lakini kwa kuwa tumekuwa tukiimba wimbo mmoja wa kutaka soka letu lisonge mbele na vijana wenye vipaji kuendeleza vipaji vyao tulikuwa na rai.

Pande mbili zinazozozana kuhusu suala la mchezaji huyo na hata wengine ambao wamejikuta wakisimamishwa kucheza ligi inayoendelea, lazima zikae chini na kutatua matatizo hayo mapema ili kutoa nafasi kwa vijana wetu kuendeleza vipaji vyao.

Tunashukuru Kamati ya Sheria na Haki za Wachezaji ya Shirikisho l;a Soka Tanzania (TFF) limetoa muda wa siku tatu kuanzia jana Jumatatu kwa klabu hizo mbili kuu kumaliza mzozo suala mchezaji huyo ili aweze kucheza.

Tunaamini viongozi wa Simba na Yanga, ushindani wao ni ndani ya kiwanja tu, ugomvi wao huwa ni ndani ya dakika 90, lakini malengo na mikakati katika kuona soka la Tanzania linasonga mbele ni wamoja, hivyo walimalize suala hili la Kessy ndani ya muda waliopewa. Inawezekana kuna hali ya kukomoana baina ya klabu hizo mbili, lakini ikumbukwe siku zote wapambanapo mafahari wawili ziumiazo ni nyasi.

Kessy ndiye anayeathirika katika mzozo huo ambao unaingia karibu mwezi wa tatu sasa bila kupatiwa ufumbuzi. Kitu kizuri ni kwamba viongozi wa Simba ni wazazi mbele ya Kessy, hivyo hata kama kuna mambo ambayo kijana wao huyo aliwakwaza siku za nyuma ni wakati wa kusamehe kwa kuwa mtoto akijisaidia haja kubwa kwenye kiganja hukati mkono.

Wito wetu ni kwa viongozi wa Yanga kukiri makosa kama kuna mahali waliteleza juu ya suala la Simba, badala ya kuendelea kuwa wabishi, kadhalika mabosi wa Simba kuwa wepesi wa kuupokea msamaha huo, ili tu Kessy arejee uwanjani na kuendelea kucheza, ikizingatiwa ni moja kati ya hazina kwa taifa katika mchezo wa soka.

Kuendelea kulumbana na kubishana katika suala hilo kisha muda uliowekwa katika utatuzi wa jambo hilo la Kessy itakuwa sio sawa na mchezaji huyohatatendewa haki.

Tunadhani muda ambao amekuwa nje ya uwanja kwa sababu ya sakata hilo ni somo na adhabu tosha kwake na huenda akajifunza, ili mchezaji afanikiwe ni lazima awe na busara na kuepuka kuendesha mambo kwa jazba na ushabiki.

Tunarudia kuzisihi Simba na Yanga na klabu nyingine kumaliza mizozo inayowahusu wachezaji wao ili kuwapa nafasi vijana waendelee kucheza, ila kila upande ujifunze kuwa siku zote mambo huyaendeshwi kienyeji bali yana utaratibu wake ambao unapaswa kuzingatiwa kwa mustakabali wa soka letu.