Simba: MO? Haondoki ng’o hata mfanye nini

SIMBA wamepata taarifa za serikali kupitia Baraza la Taifa la Michezo Tanzania (BMT) kupiga marufuku mchakato wa mabadiliko ndani ya timu hiyo pamoja na kwa watani zao, Yanga na kuchukua hatua za haraka kuona namna ya kuokoa jahazi.

Bilionea Mohammed Dewji ‘MO’ alitangaza nia ya kuwekeza Sh 20 bilioni klabuni hapo na mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo tayari yameanza kutoka mfumo wa wanachama kwenda wa Hisa, lakini BMT imepiga marufuku mabadiliko hayo ya kimfumo jambo ambalo limezua taharuki kubwa Msimbazi.

Katika kufahamu kuwa MO amekuwa mhimili mkubwa ndani ya timu hiyo kwa sasa akitoa fedha katika maeneo kadhaa, Simba imepanga kufanya mambo mawili makubwa ili kuhakikisha bilionea huyo hachepuki na anaendelea kuwapiga tafu kama kawa.

Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele alisema kwanza wanatazama kama kuna uwezekano wa kumpa MO nafasi ya kuwa mdhamini wa timu hiyo kwa wakati huu ambao, wanasubiri kuona mchakato wa mabadiliko unakwendaje.

Pia, wamepanga kukutana na serikali ili kufahamu ni kitu gani wamekosea katika mchakato wao wa mabadiliko huku Kamati ya Utendaji ikipanga kukutana hivi karibuni kuona namna ya kuendelea mbele hasa baada ya tamko la BMT.

“Kwanza wanachama na wapenzi wetu wasipaniki kuwa MO anaweza kuondoka, hapana, MO ni mwanachama wetu na ni mlezi wa timu sasa hivyo hawezi kuondoka,” alisema Kahemele jijini Dar es Salaam, jana. “Tunatazama kitu cha kufanya kwa sasa ila tunaweza kumpa nafasi ya kuwa mdhamini kwa miezi sita ama mwaka mmoja wakati tukitazama huu mchakato unakwendaje.

“Unajua tulisitisha mazungumzo na wadau wengine kutokana na huu mchakato wa mabadiliko, ambao ni muhimu sana.

“Kamati ya Utendaji itakutana kujadili muafaka wa muda mrefu, tutakutana pia na serikali ili kuona ni wapi tunakosea katika mchakato wetu, tunataka watuelekeze, tutakuwa pia na mkutano wa wanachama,” alifafanua mtendaji huyo. “Kuhusu malipo ya mishahara sidhani kama ataacha kutusaidia kulipa kwa sababu amekuwa akitoa fedha hizo kama mkopo, tunatarajia mambo yatakwenda vizuri,” aliongeza Kahemele.