Serengeti Boys yajishika Fifa

Wachezaji wa timu ya Serengeti Boys

Muktasari:

  • Awali, TFF ilipeleka suala hilo Shirikisho la Soka Afrika (Caf) ambayo iliamua mchezaji huyo apelekwe mjini Cairo, Misri kwaajili ya kufanyiwa vipimo vya MRI ili kubaini umri wake halisi lakini Wakongo hao wakapiga chenga.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeamua kuikomalia timu ya taifa ya Congo Brazzaville kuwa ilimchezesha kijeba, Langa Percy katika timu yao ya vijana chini ya miaka 17 na sasa suala hilo limepewa baraka na Fifa.

Awali, TFF ilipeleka suala hilo Shirikisho la Soka Afrika (Caf) ambayo iliamua mchezaji huyo apelekwe mjini Cairo, Misri kwaajili ya kufanyiwa vipimo vya MRI ili kubaini umri wake halisi lakini Wakongo hao wakapiga chenga.

Hata hivyo taarifa kutoka TFF zilieleza kuwa sasa Fifa imeamuru kuwa mchezaji huyo apimwe na majibu yatumwe kwenye shirikisho hilo ili kujiridhisha kwa kuwa timu nne zitakazotinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ya vijana zitafuzu moja kwa moja kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa timu za vijana chini ya miaka 17.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema kutokana na mwongozo huo wa Fifa sasa wanasubiri siku ya kwenda kumpima mchezaji huyo ili Serengeti Boys iweze kupata haki yake.

“Tumepata baraka za Fifa kwamba huyu mchezaji lazima akafanyiwe vipimo, angalau sasa tumeanza kupata matumaini ya haki,” alisema Lucas.

Hata hivyo kumekuwa na taarifa mbalimbali kutoka nchini Congo Brazzaville kwamba Percy amefariki kutokana na vita vinavyoendelea nchini humo lakini ipo walakini kama taarifa hizo ni za kweli ama zinatengenezwa kwa lengo la kulizika sakata hilo.