Serengeti Boys kujipima kwa Guinea, Rwanda

Muktasari:

  • Wakati huohuo, TFF imesema wiki ijayo itatangaza utaratibu wa Watanzania kuichangia Serengeti Boys.

Dar es Salaam. Timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya miaka 17, Serengeti Boys itacheza michezo minne ya kujipima nguvu kati ya Machi 13 hadi April 12 kabla ya kwenda nje ya nchi kuweka kambi ya mwezi mmoja kujiandaa na fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana zitakazofanyika Gabon kuanzia Mei 21 hadi Juni 5.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas amesema mechi hizo ni mbali ya ratiba ya michezo ya mitatu ya kirafiki itakayopigwa wakati  timu itakapoweka kambi nje.

"Hii ni program ya kocha na tayari tumeomba kwa wenzetu Guinea, Kenya, Rwanda na Burundi. Tunakusudia mechi hizo zitachezwa Dar au kwenye miji mingine mikoani," amesema Lucas.

Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Soka la Vijana cha TFF, Kim Poulsen amesema kucheza mechi nyingi za kujipima nguvu kutaisaidia Serengeti Boys kutimiza lengo la kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.

 

Wakati huohuo, TFF imesema wiki ijayo itatangaza utaratibu wa Watanzania kuichangia Serengeti Boys.

"Tuko kwenye mazungumzo na wenzetu wa kampuni za simu ili kupata namba moja itakayotumiwa na Watanzania kuchangia. Timu hii haina ufadhili na kama kila Mtanzania atachangia Sh1,000  kwa mfano, tutafanikiwa kuiandaa timu vizuri," amesema.

Serengeti Boys imefuzu kwa mara ya kwanza Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana baada ya kushinda rufani yake dhidi ya Congo Brazaville.

TFF ilimkatia rufani mchezaji wa Congo, Langa-Lesse Bercy kuwa amezidi miaka 17 na Shirikisho la Soka Afrika, CAF lilitoa nafasi kwa nchi hiyo kumpeleka Cairo akapimwe lakini Congo haikufanya hivyo.

Ilitoa nafasi tena kwa Congo kumpeleka Gabon wakati wa fainali za Afcon, pia Congo haikufanya hivyo ndipo Caf ikaipa nafasi Tanzania.

Tanzania iliifunga Congo mabao 3-2 mchezo wa kwanza na Bercy kufunga bao pekee katika mchezo wa marudiano. Hata hivyo, Caf iliyafuta matokeo hayo.