Samatta mdogomdogo kinaeleweka

Muktasari:

Ndani ya kipindi cha miaka miwili sasa, Samatta amekuwa akipata mafanikio zaidi mwezi huo, kabla na hata baada ya kujiunga na Genk. Mapema mwaka jana, Samatta alitangazwa mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani kwa mwaka 2015,tuzo ambayo aliipata mwezi huo baada ya kuwashinda Muteba Kidiaba na Baghdad Bounejdah.

STRAIKA namba moja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anayechezea RCK Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta ameonekana kung’ara zaidi mwezi Januari kulinganisha na miezi mingine.

Ndani ya kipindi cha miaka miwili sasa, Samatta amekuwa akipata mafanikio zaidi mwezi huo, kabla na hata baada ya kujiunga na Genk. Mapema mwaka jana, Samatta alitangazwa mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani kwa mwaka 2015,tuzo ambayo aliipata mwezi huo baada ya kuwashinda Muteba Kidiaba na Baghdad Bounejdah.

Mwezi huo huo wa Januari mwaka jana, Samatta alijiunga na RCK Genk kutoka TP Mazembe, na kuweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu Ubelgiji. Kama ilivyokuwa mwaka jana, nyota hiyo imeendelea kumuwakia Samatta mwaka huu, ambapo amefanikiwa kwa mara ya kwanza kucheza kwa dakika nyingi kwenye mechi tatu mfululizo za klabu hiyo, jambo ambalo halikuwahi kutokea tangu alipojiunga na timu hiyo.

Samatta amecheza kwa dakika 261 ndani ya mechi tatu alizocheza ndani ya Genk, ambazo ni nyingi zaidi kwake kucheza tangu alipojiunga na timu hiyo, ambapo ndani yake amecheza kwa dakika 90 katika mechi mbili mfululizo za mashindano dhidi ya Eupen na Oestende huku akifunga bao moja.

Mshambuliaji huyo aliuambia mtandao wa Genk kuwa: “Nadhani bao nililofunga litasaidia kunijengea hali ya kujiamini. Suala la kutofunga hutokea tu kama inavyotokea kwa binadamu wengine licha ya juhudi kubwa ninayofanya mazoezini. Kikubwa tunachokitazama ni timu kupata ushindi pasipo kujali kuwa ni mimi ndiye nimefunga hilo bao au mwingine.”