Redondo tayari, Juma Kaseja apata ulaji

Kipa wa Mbeya City, Juma Kaseja

Muktasari:

MBEYA City imeimarisha kikosi chake kwa kumwongeza mkataba kiungo wao, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ huku wakimsubiri kipa Juma Kaseja ambaye bado yupo jijini Dar es Salaam akiwa na majukumu ya kuwanoa makipa wa Serengeti Boys.

MBEYA City imeimarisha kikosi chake kwa kumwongeza mkataba kiungo wao, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ huku wakimsubiri kipa Juma Kaseja ambaye bado yupo jijini Dar es Salaam akiwa na majukumu ya kuwanoa makipa wa Serengeti Boys.

Wengine walioongezewa mikataba ni Haruna Shamte na straika kutoka Burundi, Hemed Murutabose.

Iwapo City wataridhishwa na kiwango cha straika huyo kutoka klabu ya Lydia Ludic Sports inayoshiriki Ligi Kuu Burundi, basi ni wazi kwamba nafasi ya Didier Kavumbangu haitakuwepo tena ingawa imedaiwa kuwa mchezaji huyo wa zamani wa Azam alikuwa akifanya mazungumzo na uongozi wa City baada ya dili lake la Vietnam kushindikana baada ya awali kushindwa kufikia makubaliano kwani alitaka apewe Dola 40,000.

Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe aliliambia Mwanaspoti kuwa wamempa mkataba wa mwaka mmoja Redondo baada ya kupokea mapendekezo ya kocha wao Kinnah Phiri huku wakimsubiri Kaseja ambaye amedaiwa kupata udeiwaka Serengeti Boys kwani kocha wa makipa wa timu hiyo, Mwalami Mohamed atahudhuria kozi ya makocha wa makipa itakayoanza hivi karibuni.

Kimbe alisema Kaseja ametoa taarifa hiyo baada ya kufikia makubaliano ya kuongeza mkataba hivyo hawana wasiwasi juu yake ingawa amekuwa akitajwa pia kwenye usajili wa makipa ndani ya kikosi cha Simba kwani kocha wao Joseph Omog amewataka viongozi waongeze kipa mmoja mzoefu.

“Redondo tumemalizana naye na yupo kambini, pia Haruna Shamte naye yupo hapa kwa ajili ya kusaini mkataba mpya, bado Kaseja ambaye tumezungumza naye na kukubaliana kuwa atakuja kusaini akimaliza majukumu yake aliyotueleza, hatuna wasiwasi naye hata kidogo, huyo Mrundi yupo kwa ajili ya majaribio kocha akimkubali tutamsajili,” alisema Kimbe.

Hata hivyo, usajili wa Shamte jana Jumatano huenda uliingia dosari baada ya Simba kuingilia kati kwa kufanya mawasiliano na beki huyo kabla ya kumwaga wino Mbeya City huku wakimshawishi kutosaini mpaka wao wafikie muafaka ambapo viongozi wa City nao wakifanya kila mbinu kuhakikisha wanampa mkataba mpya.

Mbeya City ambayo imeweka kambi yake Matemba imemsajili pia Mohamed Mkopi kutoka Prisons, Zahir Rajabu kutoka Stand United na kipa Fikirini Bakari wa Coastal Union.