Real Madrid yamaliza ukame wa miaka 5 La Liga

Muktasari:

Ronaldo ameendelea makali yake katika mchezo huo wa mwisho kwa kufunga bao kwanza katika dakika ya pili.

Madrid, Hispania. Real Madrid na Cristiano Ronaldo wamemaliza ukame wa miaka mitano baada ya kupoka ubingwa wa La Liga kutoka kwa mahasimu wao  Barcelona katika siku ya mwisho.

Vijana wa Zinedine Zidane walijihakikishia kumaliza wakiwa mbele kwa pointi tatu zaidi baada ya kuifunga Malaga kwa mabao 2-0 katika siku ya mwisho pamoja na Barcelona kuwafunga Eibar mabao 4-2.

Ronaldo ameendelea makali yake katika mchezo huo wa mwisho kwa kufunga bao kwanza katika dakika ya pili.

Kiungo Isco alitegeneza bao la kwanza kwa kupenya ngome ya Malaga na kupitisha pasi ndefu kwa Cristiano Ronaldo aliyemtoka kipa Carlos Kameni na kufunga bao la kuongoza kabla ya Karim Benzema kufunga bao la pili.

Wachezaji wa Real mwisho wa mchezo huo walivaa jezi yenye namba 33, wakimanisha hilo ni taji la 33 La Liga baada ya kusubili kwa miaka mitano.

Madrid tayari wametwaa taji la Ulaya la Super Cup pamoja na Kombe la Dunia la Klabu msimu huu.

Kwenye Uwanja wa Camp Nou, Barcelona ilione nafasi yao ya kutwaa ubingwa ikipotea baada ya kiungo Mjapani Takashi Inui akifunga bao katika dakika ya saba na 61.

Barcelona ilipata bao la kwanza la kujifunga mwenyewe beki wa Eibar, David Junca katika dakika 63rd, na Luis Suarez alisawazisha dakika 73, baada ya Lionel Messi kukosa penalti.

Messi kinara wa ufungaji wa ligi hiyo akiwa na mabao 37, alifunga bao la tatu kwa penalti nyingine dakika 75.

Eibar ilipata pigo dakika 74 baada ya beki wake Ander Capa kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

Mechi hiyo ya Camp Nou ilikuwa ya mwisho kwa kocha Barcelona, Luis Enrique uwanjani hapo baada ya kutangaza kustaafu kuifundisha timu hiyo.

Barcelona itacheza mechi yake ya mwisho ya Kombe la Mfalme dhidi ya Alaves Jumamosi ijayo.