Prisons, Mbeya City kiingilio Sh1000

Mbeya. Uongozi wa Chama cha Soka, Mbeya (Mrefa), umesema kiingilio cha mechi kati ya Tanzania Prisons na Mbeya City inayochezwa leo jioni ni Sh1,000  badala ya bure kama ilivyokuwa imetangazwa  jana baada ya kuahirishwa kwa mchezo huo.
Msimamizi wa kituo cha Mbeya, katika mchezo huo, Selemani Kharoub alisema awali baada ya kuahirishwa kwa mechi hiyo jana kutokana mvua kubwa ya mawe iliyoanza dakika 10 kabla ya mechi kuanza na mashabiki waliokuwa wameingia kutangaziwa kwamba mechi itachezwa leo, lakini hakutakuwa na kiingilio.
Anasema ‘Ni kweli jana ile tulitangaza vile kwamba itakuwa bure, lakini kama ulivyoona watu walivyotaharuki kutaka kujua hatima ya fedha zao walizotoa halafu mechi ikaahirishwa.
"Tulichukua uamuzi ule harakaharaka ikiwa ni njia pia ya kuwaondoa watu uwanjani, lakini baadaye tulivyowasiliana na viongozi wa makao makuu wakashauri kwa vile jambo lililotokea lilikuwa nje ya uwezo wetu, tunaomba mashabiki leo wataingia kwa kiingilio cha Sh1,000 badala ya bure kabisa,”  anasema Kharoub.
Anasema isingiwezekana mashabiki waingie bure kabisa kwani gharama za kuendeshea mechi hiyo ni kubwa tofauti na fedha walizopata jana, hivyo wakashauriana walau mashabiki wachangie kiasi hicho, ili kupunguza kiasi cha gharama za mchezo ikiwamo kuwalipa posho waamuzi.