Pluijm asepa na mamilion yake

Monday March 20 2017

 

By DORIS MALIYAGA

KOCHA Mholanzi, Hans Pluijm baada ya kukamata mamilion ya usajili kutoka klabu ya  Singida United, juzi Jumamosi alikwea zake pipa na kwenda zake Ghana kwa mapumziko na atakaa huko kwa wiki mbili.

Na atakaporudi, atakuwa na programu maalumu kwa wachezaji wote waliopandisha timu lengo ni kuwaangalia atakaobaki nao msimu mpya na atakaowaacha ili aendelee na usajili wa wachezaji wengine wapya.

Akizungumza na Mwanaspoti Katibu Mkuu wa Singida, Abdulrahman Sima alisema; “Ni makubaliano na atarudi baada ya wiki mbili ambapo, atakuwa na programu maalumu na wachezaji waliopandisha timu ili awatambue, baada ya hapo ataangalia wa kuwaacha na atakaowabakisha ili aanze kazi ya usajili wachezaji tayari kwa msimu mpya.”

Kwa upande wa Pluijm amesema, anakwenda kupumzika na ataanza mipango hiyo mipya mara tu atakaporejea:

“Nakwenda kupumzika na nitakaporudi ndiyo tutaanza mpango mpya wa usajili na kuisuka timu upya kwa ushindani.”

Singida iliyopanda Ligi Kuu msimu huu mbali na kuwa na wachezaji wenye majina makubwa ligi kuu, tayari imemsainisha kiungo, Mzimbabwe aliyekuwa akiichezea Chicken Inn ya nchini humo,  Tafadzwa Kutinyu.