Pluijm alizwa ndiga lake jipyaaa

Friday February 17 2017Hans PLUIJM

Hans PLUIJM 

By DORIS MALIYAGA

MZUNGU wa Yanga, Hans Pluijm ni kama ameanza vibaya mwaka 2017 kwani akiwa ameondolewa katika nafasi yake ya ukocha na kutupwa kwenye cheo cha ukurugenzi wa ufundi juzi usiku amejikuta akilizwa gari lake jipya.

Kocha huyo aliyeipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Bara misimu miwili mfululizo aliibiwa gari hilo aina ya Toyota Harrier akiwa nyumbani kwake Oysterbay, Dar es Salaam.

Alisema gari hilo alikabidhiwa hivi karibuni na kupiga nalo misele katika safari zake za hapa na pale, lakini usiku wa juzi wezi walifanya yao kwa kuliiba na mwenyewe kuja kustuka asubuhi alipoamka.

“Nimepata matatizo usiku wa kuamkia leo (jana), nimeibiwa gari niliyokuwa naitumia ikiwa nyumbani kwangu Oysterbay na inawezekana wezi waliliiba karibu kunakucha,” alisema na kuongeza: “Nimetoa taarifa kwa wahusika na kuripoti polisi ili uchunguzi ufanyike na wao wametuambia tusubiri wafanye kazi yao,” alisema Pluijm ambaye ana uzoefu na soka la Afrika baada ya kufanya kazi kwa miaka mingi nchini Ghana.

Kaimu Katibu Mkuu wa zamani wa klabu hiyo, Baraka Deusdedit alikiri juu ya kuibiwa kwa gari la kocha huyo, lakini hakutaka kulizungumza kwa undani tukio hilo kwa madai kwamba yeye si msemaji.