Pluijm: Msijidanganye nyie, mtaumia Taifa

Kocha Han Pluijm

Muktasari:

  • Kelele na vicheko hivyo vya Simba zilishamfikia mapema Kocha Han Pluijm, ambaye alipozisikia akacheka sana na kuwataka kamwe wasijidanganye wataumia vibaya sana.

KIPIGO cha bao 1-0 ilichopewa Yanga na Stand United juzi Jumapili kimewapa kiburi Simba, watapita mitaani wakijipiga kifua huku uso ukichanua kwa tabasamu pana kwa kuamini watakuwa na kazi nyepesi Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa.

Hata hivyo, kama Simba walikuwa hawajui ni kwamba Yanga mapema jana asubuhi walikwea ‘mwewe’ kutoka Shinyanga kisha kutua Dar kabla ya kusepa zao kuweka kambi visiwani Pemba. Na kama hawajui ni kwamba asubuhi hii kabla watu hawajapiga mswaki ili kupata kifungua kinywa, Yanga ilikuwa Uwanja wa Gombani ikijifua kumwinda mnyama Simba.

Kelele na vicheko hivyo vya Simba zilishamfikia mapema Kocha Han Pluijm, ambaye alipozisikia akacheka sana na kuwataka kamwe wasijidanganye wataumia vibaya sana.

Akizungumza na Mwanaspoti Pluijm alisema kama kuna watu wanaodhani kwamba, kupoteza kwao mchezo wa juzi ni kiashiria kuwa pia watapoteza mchezo dhidi ya Simba basi watakuwa wanajidanganya na kwamba, watashuka Taifa na hasira zote.

Kocha Pluijm akiwa katika akili zake timamu, huku akiwa na uso wa kawaida amesema ameishuhudia Simba katika mechi zao zisizopungua nne msimu huu na kujua mbinu zao zote katika utawala wa Kocha Mcameroon Joseph Omog na kwamba, hiyo itakuwa mecho tofauti na watu wanavyofikiri.

Mzungu huyo aliyebeba pointi sita na mabao manne katika mechi mbili dhidi ya Simba msimu uliopita, alisema anachoweza kukikubali kwa Simba ni kuwa wamekuwa na mabadiliko kidogo na kuanza kucheza kitimu, lakini akili yake inamwambia hata wao wanaiogopa Yanga, licha ya kujichekesha mitaani.

MSIKIENI MWENYEWE

“Hii mechi ya Stand ni mchezo tofauti na ule dhidi ya Simba na kama kuna anayefikiria kwamba, matokeo haya ya kupoteza kwetu yatakuwa na mchango wowote katika mchezo ujao, naona atakuwa anajidanya mwenyewe na hiyo ni juu yake,” alisema.

Pluijm alisema anajua mbinu zote za zitakazomuwezesha kuondoka na pointi tatu katika mchezo huo ambapo, hata kikao alichofanya na wachezaji wake wamemshusha presha wakiusubiri mchezo huo kwa hamu kubwa.

“Binafsi nadhani hata Simba wanaiogopa Yanga, hiyo itakuwa ni mechi tofauti kabisa nimewaona Simba ni timu iliyoanza kubadilika, lakini kila kitu chao nakijua nafikiri watu wasubiri matokeo ya mwisho siku hiyo.

“Tuna timu imara na kilichotokea juzi ni sehemu ya matokeo ya soka tulifanya kosa moja tukapoteza, lakini tulitengeneza nafasi nyingi, kwa sasa sitaki tena kuzungumzia kuhusu viwanja sio hoja mpya, nina kila taarifa za Simba ya sasa zinanitosha.

“Jambo lililonivutia ni kuwa wachezaji wangu wanajua umuhimu wa mchezo huo hivyo, tunachohitajika kukifanya ni kujua kucheza kwa akili na kuheshimu nidhamu ya mchezo tuna kikosi imara na halitakuwa jambo jipya tukishinda,” alisema.

Simba ipo kileleni kwa sasa na pointi zao 16, huku Yanga ikiwa na alama 10 na pungufu ya mchezo mmoja ikikamata nafasi ya tatu kwa sasa nyuma ya Stand Utd.