Pasi za kiungo mpya hadi aibu

HABARI mbaya ambazo zitawashtua mashabiki wa Yanga ni kwamba klabu ya AC Leopards ya Congo Brazzaville, imesikia mipango ya Kocha George Lwandamina ya kumnyatia straika Mzambia,Winston Kalengo wakampiga pini.

Yanga walishafanya mazungumzo na mchezaji huyo anayesifika sana Zambia na Congo Brazzaville baada ya kuona mavitu yake kwenye video zilizoko kwenye mtandao wa Youtube na wakakubaliana na Lwandamina asilimia zote kwamba kijana atue nchini wikiijayo. Lakini wakati akijiandaa kurudi kwao Zambia kwa likizo ili aunganishe Dar es Salaam moja kwa moja, Wakongo wakashtukia wakamuita mezani wakampandia dau la usajili pamoja na mshahara, akashindwa kutamka neno zaidi ya kutia saini halafu baadaye akawatumia meseji Yanga: “Nimeshindwa kukataa ofa ya Leopards, ni kubwa mno.”

Lakini sasa Yanga imehamishia akili kwingine na kabla Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli hajahudhuria sherehe za Uhuru Desemba 9, Yanga watakuwa wameshajua mashine mpya inayokuja Jangwani.

Yanga tayari imeingia mkataba na kiungo mkabaji, Justine ambaye alianza kazi rasmi jana Ijumaa na kwenye mazoezi ya jioni alikuwa kivutio kikubwa, alitumia umahiri na umbo lake kufanya vitu adimu. Jangwani.

Katika mazoezi hayo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam ambao hutumiwa zaidi na matajiri, katika mazoezi ya dakika 15 ya pasi na kukaba wachezaji waligawanywa kwenye makundi ya watu saba saba ambapo Zulu alipiga pasi 38 zilizowafikia walengwa huku akipoteza tisa tu. Kocha alipoona mzuka umempanda akamwambia: “Kaa pembeni nenda kapashe.” Ndipo akapewa zoezi la kukimbia kwa muda.

Awali, aliomba jezi namba ambayo kwa kawaida ni ya Twite lakini akanyimwa akapewa namba 14 iliyokuwa inavaliwa na Mniger, Youssouf Boubacar ‘Diego’ ambaye alitemwa. Lakini kwa kuondoka Twite inamaanisha kwamba atapewa jezi namba 6 rasmi.

 

Lwandamina na mchujo

Kiraka mwenye nguvu za mikono kuliko beki yeyote katika Ligi Kuu Bara, Mbuyu Twite ameachwa rasmi jana baada ya kuitwa na Mkurugenzi wa Ufundi, Hans Pluijm pamoja na Katibu Mkuu, Baraka Deusdedit. Twite alisema: “Waliniita wakaniambia kwamba mimi ni mchezaji huru naweza kutafuta klabu yoyote kwa sasa.”

Lakini kocha Lwandamina amesema kuna dakika 90 za kuamua yupi anatemwa yupi anabaki. “Sijaamua nani anachwa hapa ningependa kila mchezaji aonyeshe kiwango chake bila kujali hizo taarifa wakati ukifika tutafanya maamuzi kwa kuisadia Yanga, nasikia tu kuna taarifa kwamba huyu ataachwa lakini nimeomba kuna mechi niandaliwe ili niweze kujiridhisha zaidi sitaki kufanya uamuzi wa haraka katika eneo hili.”

Mbuyu Twite ambaye alithibitisha kutemwa jana aliongeza kwa kusema: “Sina tatizo kama nitaondolewa najua mkataba wangu uko ukingoni, lakini hii ni timu ninayoipenda ndiyo maana nimekuwa nikiitumikia kwa nguvu, binafsi najiona bado nina nguvu, lakini maamuzi ya mwisho ni yao uongozi.”

 

Wakongo waharibu dili

Kalengo aliifafanulia Mwanaspoti jana: “Nimeshindwa kuja kujiunga na Yanga, ni timu nzuri ina jina kubwa lakini kuna mambo yamefanya nikubali kubaki hapa hasa ni masilahi, nipo katika harakati za kurudi nyumbani Zambia kutulia kidogo kabla ya kurudi kujiandaa na ligi msimu mpya.”

Habari za ndani zinasema Yanga inaendelea kumsaka straika mkali wa kusimama na Donald Ngoma na Amissi Tambwe. Yanga sasa inasubiri dili la Vincent Bossou anayetaka kununua mkataba wake wa miezi minane uliobaki ili atimkie Vietnam, kama wakimuuza kwa wakati nafasi yake itajazwa na straika ambaye ndani ya siku chache zijazo atabainika kupitia ukurasa huu huu. Achana na redio mbao.