Owino aiumbua Yanga kweupe

OWINO

MASHABIKI wa Yanga bado wamenuna baada ya timu yao kufungwa bao 1-0 na Stand United mjini Shinyanga, lakini beki Joseph Owino amezidi kuwatia hasira baada ya kufichua kuwa, kikosi hicho cha Hans Pluijm dakika zao za kucheza ni 15 tu.

Owino alisema baada ya muda huo wa Yanga kutawala soka, hukata pumzi na ndio maana haikuwa ajabu kwao kulala kwa Chama la Wana analolichezea, japo kwa sasa yupo Oman, akifukuzia dili la kujiunga na klabu ya Fanja FC.

Beki huyo Mganda aliyewahi kuzichezea Simba na Azam, alisema Yanga imekuwa ikishindwa kumudu dakika 90 za mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara kwa sababu wachezaji wao wamechoka kwa kucheza mfululizo mechi za kitaifa na kimataifa.

Alisema kwa hali hiyo kuna uwezekano watetezi hao wakashindwa kutetea taji lao msimu huu kutokana uchovu walionao, huku akisema timu pinzani zitakazokutana na Yanga zikishindwa kutumia vizuri dakika 75 za mwisho baada ya zile 15 za mwanzo basi hawawezi kuifunga tena. “Nafurahi kuona Stand inafanya vizuri, japo sipo kwenye kikosi kwa sasa, niliwaona Yanga kwenye mechi zao zilizopita ni timu ambayo ina wachezaji wazuri, lakini wamechoka hawawezi kuhimili kucheza kwa muda mrefu, dakika zao ni 15 tu.

“Hakuna binadamu asiyechoka, Yanga hawajapumzika kabisa tofauti na timu zingine, wamecheza mechi nyingi mfululizo hilo ni tatizo ambalo litawafanya msimu huu washindwe kutetea hata ubingwa,” alisema Owino.

Pia aliweka wazi kuwa bado ana nafasi ndani ya kikosi cha Stand hasa baada ya kuwepo na taarifa za kuondoka kwa kocha Patrick Liewig raia wa Ufaransa;

“Nilimuaga Liewig kuwa nakuja huku kujaribu bahati, ila naye aliniaga anaondoka. Liewig ni kocha mzuri na anajua kugundua vipaji na kumbadilisha mchezaji. Miaka yote nilikuwa nacheza kama beki sikuwahi kufikiria kucheza namba nyingine ila tangu niingie Stand United, amekuwa akinichezesha namba sita na nane.

“Nilijikuta nafurahia kucheza nafasi hizo mbili wala sikutamani kurudi kucheza namba niliyokuwa nimeizoea (beki wa kati), kama nitarejea Stand na kukuta kocha mwingine basi itanibidi niendane na mfumo wake,” alisema Owino.