Owino achemka, Liewig abakizwa

Muktasari:

Stand pamoja na mambo mengine umetaka kulipwa dola 3,500 ambazo walitumia kumpangia makazi na ada ya TFF dola 2,000.

WAKATI uongozi wa Stand United ukimtuliza kocha wao Patrick Liewig kubaki hadi mwisho wa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu, beki wao Joseph Owino amekwaa kisiki nchini Oman, amefuzu kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Fanja, lakini uongozi wake umegoma kutoa barua ya kumwacha ukitaka ulipwe kwanza mamilioni ya shilingi kama gharama za kumruhusu kujiunga na klabu hiyo.

Stand pamoja na mambo mengine umetaka kulipwa dola 3,500 ambazo walitumia kumpangia makazi na ada ya TFF dola 2,000.

Wiki iliyopita uongozi wa Stand kupitia Katibu wao, Kennedy Nyangi ulithibitisha kuwa Liewig anayesimamiwa na mwanasheria wake Franck Nicolleau, ambaye pia ni Mfaransa kusaini mkataba wa makubaliano ya kuvunja mkataba huo na kulipwa dola 10,000 na si vinginevyo badala ya kulipwa mshahara wa mwezi mmoja kama walivyoomba viongozi wa Stand United.

Liewig alitakiwa kusaini mkataba huo Jumatatu au juzi Jumanne, lakini walikaa chini na kuangalia upya mahitaji ya kikosi chao ambacho kinashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu na kukubaliana tena kuwa aendelee kuwepo hadi mzunguko utakapomalizika. Liewig anaondoka leo Alhamis kuifuata timu yake Songea ilikokwenda kucheza na Majimaji.

Wakati Liewig akikubali kuondoka, Owino naye atalazimika kurudi Stand United baada ya kushindwa kupata barua itakayomruhusu kuichezea Fanja hadi hapo Stand watakapolipwa dola 5500 kwanza.

Owino aliliambia Mwanaspoti kuwa; “Narudi Stand kwa sababu hawataki kunipa barua ya kuniachia, makubaliano yetu nikipata timu nitaruhusiwa kucheza lakini sasa wamegeuka na hawataki kunipa uhamisho.

“Pesa yangu ya usajili sijalipwa mpaka leo, nimekuja kutafuta maisha wananivurugia kwa kweli nashindwa kuelewa, nitarudi huko ila sitacheza maana huku kila kitu nimekifanya ikiwemo kusaini mkataba ilibaki barua tu kutoka huko,” alisema Owino

Mratibu wa Stand, Mbasha Matutu naye akifafanua kuhusu hilo; “Hatujamzuia Owino kucheza huko ila tumeutaka uongozi wa Fanja kuwasiliana nasi kwa kuwa kuna gharama tulizifanya kwa Owino ambazo ni ada ya TFF kwa wageni pamoja na kodi ya makazi. Wakilipa hizo pesa basi tunamtumia barua haraka sana.

“Alipoondoka aliniaga na nilimwambia akamuage kocha wake naye aliruhusu alipofika kule walihitaji nakala ya mkataba wake, vitu vyote nilivifanya na kumtumia iweje leo hii nimzuie kucheza huko? Ni muhimu taratibu zifuatwe na ikishindikana basi arudi kuichezea Stand hadi mkataba wake utakapomalizika ataondoka kwani, hatuna nia mbaya na wachezaji wetu,” alisema Mbasha

Owino alisaini mkataba wa mwaka mmoja na Stand United kwa makubaliano ya Sh 10 milioni ambazo hajalipwa kabisa ingawa hata huko Fanja amesaini mkataba kwa makubaliano ya kulipwa baadaye watakapoanza kucheza kwa kuwa klabu hiyo kwa sasa imeyumba kiuchumi na kushindwa kufanya fujo kwa kumwaga mkwanja kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.