Owino, Stand wafikia pabaya

JOSEPH OWINO

BEKI wa Stand United, Joseph Owino amesema kuwa endapo uongozi wa klabu hiyo utashindwa kuvunja mkataba wake basi suala hilo atalipeleka Fifa ambao watamruhusu kuondoka ili acheze timu nyingine na kumlipa fidia.

Owino alisaini mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo yenye masikani yake mjini Shinyanga wenye thamani ya Sh 10 milioni ambazo hawajamlipa hadi sasa ikiwemo mishahara ya miezi miwili.

Owino aliliambia Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka jijini Kampala kwamba aliwaomba wavunje mkataba wake ili awe huru na kwenda kucheza timu nyingine yenye uwezo wa kumlipa ingawa tayari alikosa nafasi ya kucheza timu ya Fanja FC ya Oman iliyoonyesha nia ya kumsajili lakini uongozi wa klabu hiyo ulishindwa kumwachia kwa kutaka walipwe Dola 8,500.

Owino alisema kuwa, maisha ndani ya Stand United yamekuwa magumu tofauti na alivyofikiria wakati huo timu hiyo ikiwa na udhamini wa Kampuni ya Acacia.

“Nashangaa hata barua yangu ya kuvunja mkataba wanasuasua inaonyesha kwamba hawako tayari, niliwaandikia barua ili mkataba uvunjwe niwe huru kwani hawana pesa za kunilipa, maisha ya pale ni magumu na siwezi kuendelea kuwepo huku nikiumia.

“Ila kama wataendelea kunisumbua basi hili suala litafika Fifa ambao wataamua na watalipa pesa nyingi kuliko hivi ambapo nawabembeleza mimi sielewi hawa viongozi kitu gani kinawafanya wanisumbue na tushindwe kuelewana.

“Kwanza naamini Fifa watatoa barua ya mimi nicheze timu nyingine kulinda kiwango changu ndipo mambo mengine yataendelea kwani kuvunja mkataba kwa amani hawataki,” alisema Owino.

Owino alisema tayari amemtafuta mwanasheria wake wa kusimamia jambo hili endapo litaendelea kuwekewa ugumu ili aanze kufuata taratibu za kisheria: “Mimi na meneja watu tulikaa chini na kuamua kuandika barua ya kuvunja mkataba kwa amani ila sasa tumemtafuta mwanasheria ili asimamie maana tunaona dalili za kusumbuana.’’

Msemaji wa Stand United, Deo Kaji Makomba alisema kuwa bado suala la Owino linajadiliwa na hivyo makubaliano yakifikiwa mkataba wake utavunjwa.