Omog aipotezea Yanga kimtindo

KOCHA Mkuu wa Simba, Mcameroon Joseph Omog amesema kitendo cha timu yake kuongoza ligi ni dalili njema ya kutwaa ubingwa wa msimu huu huku akifafanua kuwa mechi yao na Yanga haimuumizi kichwa kwani, amejiandaa kikamilifu.

Simba inaongoza ligi na pointi  13 baada ya kucheza mechi nne, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 10 sawa na Azam FC inayoshika nafasi ya tatu, huku Yanga ikiwa imecheza mechi tatu.

Ameliambia Mwanaspoti kuwa anajua anacheza na Yanga ambao ni timu nzuri, lakini anawachukulia sawa na timu zingine kama Majimaji na Azam FC aliowachapa bao 1-0 wikiendi iliyopita.

“Yanga ni timu nzuri, lakini nawachukulia sawa na timu nyingine kama Majimaji na Azam FC na sasa nafanya kazi nzito na vijana wangu kuhakikisha tunashinda.

“Tuna mechi na Majimaji mbele yetu, lakini katika maandalizi tunajiweka tayari na mechi zote ili tusipoteze pointi hata moja,” alisema.

Akiuzungumzia ubora wa straika wa Yanga, Mzambia Donaldo Ngoma kocha huyo alisema: “Siangalii timu kwa ajili ya mtu mmoja, tutajiandaa kukabiliana na timu nzima na ninachokiamini, tutafanya vizuri, hilo ndiyo jambo la msingi kwa sasa kwenye kikosi changu.”

Kuhusu kuongoza ligi, Omog alisema: “Ni dalili njema ya kufikia malengo yetu ya kubeba ubingwa msimu huu, lakini tuna kazi nzito ya kuhakikisha hakuna atakayeweza kuing’oa”.