Omog aamua kujilipua mazima Simba

Muktasari:

“Tuna timu nzuri yenye ubora kuanzia huku nyuma katikati na hata mbele lakini tatizo tulilonalo ni uwezo wa kupambanua mambo na majukumu yao kwa baadhi ya wachezaji wangu hasa washambuliaji,”alisema Omog alipozungumza na Mwanaspoti ambalo ndilo gazeti pekee la Kiswahiili Afrika Mashariki linalochapishwa Kenya na Tanzania.

KOCHA Mkuu wa Simba, Joseph Omog ametamka kuwa yuko katika wakati mgumu kutekeleza malengo ambayo amejiwekea kutokana na mastraika kushindwa kutumbukiza mipira nyavuni lakini ameapa kwamba kama viongozi wakikubali aendelee kuwepo msimu ujao ataingia msituni kusaka straika mwenyewe mguu kwa mguu.

“Tuna timu nzuri yenye ubora kuanzia huku nyuma katikati na hata mbele lakini tatizo tulilonalo ni uwezo wa kupambanua mambo na majukumu yao kwa baadhi ya wachezaji wangu hasa washambuliaji,”alisema Omog alipozungumza na Mwanaspoti ambalo ndilo gazeti pekee la Kiswahiili Afrika Mashariki linalochapishwa Kenya na Tanzania.

Omog raia wa Cameroon alisema usajili walioufanya katika vipindi viwili vya usajili vilivyopita walitafuta washambuliaji ambao walionekana bora lakini katika hali ya kushangaza wameshindwa kufikia malengo ya mahitaji ya timu hiyo licha ya kwamba inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara na imefuzu hatua ya 16 bora ya Kombe la FA.

“Uongozi ulitafuta wachezaji wazuri lakini tatizo limekuja baadhi yao wameshindwa kufikia kile timu ilichotaka kutoka kwao kuna mambo mengi yamechangia. Timu bado ipo katika mashindano hatuwezi kukata tamaa, nimekuwa nikitumia muda mwingi kuongea na kuwapa mazoezi maalum baadhi ya washambuliaji lakini hakuna mabadiliko mfano mzuri ni Laudit (Mavugo),”alisema kocha huyo ambaye amekiri kwamba analazimika kutumia akili za ziada kuweka mambo sawa.

“Nimekuwa nikiongea naye kuhakikisha anabadilika lakini hali ya mambo inaonekana bado hajafanya kile ninachotaka,tunatengeneza nafasi nyingi lakini kuzitumia ni tatizo, hili tatizo ni kubwa kwetu, ni lazima tushirikiane kulitatua. Ndio maana tunapambana kwa nguvu zote kuhakikisha mambo yanakwenda sawa na tupate namna kukifikia hichi tunachokihitaji kwa wakati huu uliopo.

“Mungu akipenda kama tutaendelea kuwa pamoja hapa msimu ujao nataka kuushauri uongozi tutafute washambuliaji wazuri wenye ubora wa kupambana kwenye ligi ya hapa Tanzania. Ni ngumu inahitaji mtu anayeweza kujitoa mhanga kwa ajili ya timu na ambaye muda wowote anajua nini anapaswa kukifanya bila masihara,”alisisitiza kocha huyo wa zamani wa Azam anayemudu kuzungumza lugha ya Kiingereza na Kifaransa.

 

Hali ilivyo

Simba ina jumla ya washambuliaji sita ukiondoa Fredrick Blagnon aliyetolewa kwa mkopo ambao ni Mavugo, Pastory Athanas, Ibrahim Ajib, Haji Ugando, Juma Liuzio na Shiza Kichuya lakini mpaka sasa washambuliaji wa timu hiyo wamefunga mabao 17 pekee wakati viungo wakifunga mabao 13 na kufanya watofautiane kwa mabao manne pekee.

Kichuya ambaye hajafunga bao hata la kuotea tangu Novemba 2 mwaka jana kwenye mechi na Stand United, ndiye anayeongoza akiwa na mabao tisa akifuatiwa na Mavugo manne, Ajib matatu na Blagnon moja wakati viungo nao wakiongozwa na Mzamiru mabao sita, Mohamed Ibrahim manne na Jamal Mnyate matatu.

Washambuliaji wapya wawili Athanas na Liuzio bado hawajafunga bao lolote katika mechi za ligi mpaka sasa lakini Omog ana imani kubwa kwamba wanahitaji muda kwavile hawajakaa na timu muda mrefu.